Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

PROF. KAHYARARA AITAKA LATRA KUHAKIKISHA KAMPUNI ZA TIKETI MTANDAO ZINAUNGANISHA MIFUMO YAO NA YA SERIKALI
Imewekwa: 06 Jul, 2025
PROF. KAHYARARA AITAKA LATRA KUHAKIKISHA KAMPUNI ZA TIKETI MTANDAO ZINAUNGANISHA MIFUMO YAO NA YA SERIKALI

Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha wamiliki wa mifumo ya Tiketi Mtandao nchini wanaunganisha mifumo yao na Mfumo Jumuishi wa Mauzo ya Tiketi unaofahamika kwa jina la Safari Tiketi kwa kuwa ni jambo la kisheria na Kikanuni.

Prof. Kahayarara amesema hayo alipotebelea jengo la LATRA katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Dar es Salaam Julai 05, 2025. Amesema kuwa, uunganishaji wa mifumo ya tiketi mtandao na Mfumo Jumuishi wa Serikali ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nakumbuka Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa akizindua treni ya kisasa pale Dodoma, alitoa maelekezo nane na mojawapo ni hili la kuwa na Mfumo Jumuishi wa Tiketi Mtandao. Tunafurahi kwamba LATRA wameliwezesha hili na  mfumo huu unamwezesha abiria kukata tiketi za mabasi pamoja na treni za kisasa (SGR) na za reli ya kati (MGR) kwa urahisi kwa njia ya mtandao,”amesem Prof. Kahyarara.

Prof. Kahyarara ameongeza kuwa, Mfumo wa Safari Tiketi unasaidia wamiliki wa mabasi kupata mapato yao papo hapo na pia unarahisisha ufuatiliaji wa mabasi yanayotoa huduma pamoja na kufahamu idadi ya abiria wanaosafiri.

Kwa upande wake, CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema ni kosa kisheria kuwa na mfumo wa kutoa tiketi mtandao bila kuthibitishwa na LATRA, pia, ametoa tahadhari kwa wamiliki wa mabasi kutotumia kampuni za tiketi mtandao zisizoidhinishwa na LATRA baada ya tarehe 14 Julai, 2025.

“Wamiliki nawatahadharisha msije mkaingia kwenye matatizo ya kuzuiliwa kutoa huduma kwa kuwa usipotoa tiketi mtandao, huruhusiwi kufanya kazi ya usafirishaji na pia haturuhusiwi kukupa leseni. Tumewapa taarifa za awali kuhusu kampuni ambazo hazijakamilisha utaratibu kwahiyo muwafuatilie na muhakikishe mnatumia kampuni zilizokidhi vigezo mara baada ya muda waliopewa kuisha,” amesisitiza CPA Suluo.

Tarehe 02 Julai, 2025 Mamlaka ilitangaza kampuni tatu za Tiketi Mtandao ambazo mifumo yao imekidhi vigezo ambazo ni Otapp Agency Company Limited, Hashtech Tanzania Limited na Iyishe Company Limited na kampuni nyingine sita (06) ambazo ni AB Courier Express Limited, Busbora Company Limited, Logix Company Limited, Mkombozi Infotech Company, Sepatech Company Limited na Web Corporation Limited. zilizopatiwa siku 14 kushughulikia changamoto za mifumo yao ili kuidhinishwa.

Aidha Kampuni mbili  Duarani Innovative Company na Itule Company  zimebainika kuwa na changamoto na kukosa sifa za kutoa huduma ya Tiketi Mtandao na hivyo wamepewa siku (07) za matazamio na wakishindwa hawataruhusiwa kutoa huduma na wateja wao watashauriwa kuhamia kwa watoa huduma waliokamilisha utaratibu.

Kanuni ya 5 ya Kanuni za Tiketi Mtandao za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za mwaka 2024 zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 20 la Januari 12, 2024 zimeweka vigezo vya kupata kibali ambavyo ni pamoja na mfumo husika kuwa na ulinzi dhidi ya uvamizi wa kimtandao na kuwa na uwezo wa kuunganishwa na mifumo ya Serikali.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo