Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YATANGAZA NAULI KIKOMO ZA MABASI YA MIJINI NA NJIA NDEFU
Imewekwa: 09 May, 2022
LATRA YATANGAZA NAULI KIKOMO ZA MABASI YA MIJINI NA NJIA NDEFU

Na. Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) leo Aprili 30, 2022 imetangaza nauli mpya za mabasi ya safari ndefu na ya mjini zitakazoanza kutumika siku 14 kuanzia sasa.

 Akizungumza mbele ya waandishi wa habari na wadau wa Usafiri Ardhini, Mkurugenzi Mkuu LATRA Bw. Gilliard Ngewe amesema mabasi ya mijini kuanzia kilometa 0 hadi 10 nauli itakuwa shilingi 500 badala ya 400 iliyokuwa ikitumika hapo awali, na kwa safari zote za mjini kutakuwa na ongezeko la shilingi 100.

Vilevile kwa mabasi yanayoenda mikoani, Bw. Ngewe amesema kwa daraja la kawaida, kiwango cha ukomo ambacho Mamlaka imeridhia kwa abiria kwa kilometa ni shilingi 41.29 ambapo ni sawa na ongezeko la shilingi 4.40 sawa na asilimia 11.92 ambapo kiwango kilichokuwa kinatumika zamani ni shilingi 36.89 kwa abiria kwa kilometa.

Vilevile amesema, kwa daraja la kati, kiwango cha sasa kwa abiria kwa kilometa ni shilingi 56.88 ambayo ni sawa na ongezeko la shilingi 3.66 sawa na asilimia 6.88, kiwango kilichotumika hapo awali kilikuwa ni shilingi 53.22 kwa abiria kwa kilometa.

 “Kwa mujibu wa vifungu vya 27 (1) na 28 (1), (2) vya Sheria ya LATRA Na. 3 ya mwaka 2019, upande ambao haujaridhika na maamuzi ya Mamlaka unatakiwa ndani ya siku kumi nan ne (14) kukata rufaa kwa Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal) kama Sheria ya Ushindani inavyoelekeza”, amefafanua Bw. Ngewe

Vilevile Bw. Ngewe amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 19 ya LATRA ya mwaka 2020, watoa huduma wanatakiwa kutoa matangazo ya nauli mpya kwa siku kumi na nne kabla ya kuanza kutumia nauli mpya kupitia vyombo vya habari vinavyowafikia watu wengi.

Aidha, Bw. Ngewe amesema vifungu namba 5 (1) (c) (iii), 19 (2) na 21 (2) (b) vya Sheria ya LATRA Na. 3 ya mwaka 2019 pamoja na Kanuni ya 15 ya Tozo ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini ya mwaka 2020, GN. Na. 82, vinaitaka Mamlaka kupanga nauli kwa kuzingatia; Gharama za utoaji huduma ya usafiri wa mabasi,, Nauli shindanishi kwenye soko ambazo zinavutia soko, Kulinganisha nauli na mahali pengine na faida ya utoaji huduma, Maslahi ya Walaji (abiria) na watoa huduma ya usafiri wa mabasi, Kulinda mitaji ya wawekezaji pamoja na kupata maoni ya wadau

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria Na. 3 ya Mwaka 2019 ili kudhibiti huduma za usafiri ardhini katika sekta ndogo za reli, barabara na waya. Sheria ya LATRA ilifuta Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo