
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetengeneza Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaojulikana kwa jina la Safari Tiketi uliounganishwa na mifumo mingine ya utoaji tiketi ukiwemo wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) na mifumo ya tiketi za mabasi kurahisisha ukataji tiketi na kutunza taarifa sahihi za abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane Agosti 8, 2025 yaliyofanyika viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa, jambo lililowavutia watu wengi kwenye maonesho hayo ni matumizi ya Tiketi Mtandao ambapo hadi sasa jumla ya kampuni tano (5) zimekidhi vigezo na kupatiwa vibali vya kutoa huduma za tiketi mtandao baada ya kuthibitishwa na LATRA kuwa mifumo yao ni salama na imezingatia vigezo na masharti.
“Eneo hili tumeendelea kutoa msisitizo na siku za karibuni tumekuwa tukizungumzia kutoa kibali kwa makampuni au mifumo ambayo inatoa tiketi mtandao na ikumbukwe kuwa Serikali ilitoa Kanuni ya kusimamia usafiri huu ambayo ni Kanuni ya 5 ya Kanuni za Tiketi Mtandao za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za mwaka 2024 ambazo zimeweka vigezo vya kupata kibali ikiwa ni pamoja na mfumo husika kuwa na ulinzi dhidi ya uvamizi wa kimtandao na kuwa na uwezo wa kuunganishwa na mifumo ya Serikali” amesema CPA Suluo.
Kwa upande wake Bw. Frank Fredy, Meneja wa Kanda ya Kati wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) amesema kuwa, Mfumo wa Safari Tiketi umeondoa migogoro mingi ya Bima kwa kuwa na uwezo wa kutunza taarifa za abiria kwa mtumiaji wa mfumo huo ambaye anapaswa kujaza taarifa zake kwa usahihi ikiwemo majina kamili, namba ya simu na mahali apokwenda.
“Mfumo huu wa Safari tiketi umesaidia sana kutatua migogoro kati ya kampuni za bima na watumiaji wa bima, ilikuwa mtu akikosa tiketi anakosa haki ya kulipwa fidia lakini kwa sasa kwa kutumia mfumo wa safari tiketi unapata taarifa za abiria na analipwa haki yake, hili ni jambo zuri ambalo linampa mwananchi ambae angeweza kupoteza haki yake kupata haki zake za msingi, ninacho sisitiza kwa wananchi ni kwamba hakikisha unapata tiketi yako ya kielektoniki ili tatizo linapotokea safarini uweze kulipwa fidia za bima kwa urahisi” amefafanua Bw. Fredy.
Wakati huohuo Bw. Jabeer John, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wasafirishaji Mkoa wa Mwanza (UWAMWA), ameeleza kuwa chama hicho kimezindua mfumo wa Tiketi Mtandao kwenye maonesho hayo ya Nanenane ambapo abiria wa mabasi ya mijini (daladala) Mwanza anaweza kukata tiketi hiyo kwa wakala alioko karibu yake na kuitumia anapoingia na kutoka kwenye usafiri huo na kwamba utasaidia kupunguza changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwakabili watumiaji wa usafiri huo na kusaidia serikali kupata takwimu sahihi za watumiaji wa usafiri wa mijini.
LATRA itaendelea kutekeleza kwa ufasaha maagizo ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya kubuni na kutumia mifumo ya TEHAMA katika kuimarisha huduma za usafiri ardhini nchini.