
SSP Nokter Kilewa, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya amewaonya madereva wanaochezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kuacha tabia hiyo mara moja kwani wanaweza kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kufutiwa leseni zao.
SSP Kilewa amesema hayo kwenye mafunzo ya Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Agosti 06 na 07, 2025, Kituo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kilichopo Mikocheni, Dar es Salaam na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli.
“Naishukuru sana LATRA kwa kutupatia mafunzo haya ambayo yanaenda kubadilisha utendaji kazi wetu kwa kuongeza ufanisi ukizingatia baada ya mafunzo haya tumeongeza wigo wa uelewa kuhusu mfumo huu unavyofanya kazi na hivyo tunafahamu namna bora ya kuutumia kwa kufuatilia magari yakiwa barabarani ili kupunguza ajali nchini,” amesema SSP Kilewa.
Naye Bw. Geoffrey Silanda, Meneja Uratibu Usalama na Mazingira LATRA ameeleza namna mfumo wa VTS unavyofanya kazi ikiwa ni pamoja na kufuatilia na kutoa taarifa za magari kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa safari, na amebainisha faida za mfumo huo kuwa, tangu kuanzishwa kwake umesaidia kupunguza ajali zinazogharimu maisha ya watu na mali zao.
“Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuwajengea uwezo Wakuu na Warakibu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mikoa yote nchini ambapo hadi sasa, tumetoa mafunzo mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Mbeya,” amesema Bw. Silanda.
Kwa upande wake, Bw. Mbwana Ndaro, Afisa Mfawidhi LATRA Kituo cha VTS amewaeleza maafisa hao namna wanavyoweza kutumia mfumo huo kupata taarifa zote za magari na kumtambua dereva anayekiuka Sheria na Taratibu za usafiri ardhini ikiwa ni pamoja na kuendesha gari kwa mwendo hatarishi, dereva kuendesha gari zaidi ya saa nane, kuchezewa kwa mfumo na kupata taarifa iwapo gari imepata ajali kwa kutumia mfumo huo.
Vilevile Bw. Ndaro ameelezea kuhusu matumizi ya Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i-Button) kuwa, dereva anapaswa kukitumia anapowasha gari na wakati wote akiwa safarini na endapo gari litapata changamoto yoyote , ni rahisi kupata taarifa za dereva aliyekuwa anaendesha.
Mafunzo hayo ya siku mbili yametolewa na Bw. Geoffrey Silanda, Meneja Uratibu Usalama na Mazingira LATRA, Bw. Mbwana Ndano, Afisa Mfawidhi LATRA Kituo cha VTS na kuhudhuriwa na Mha. Shabani Mdende, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Mbeya, SSP Nokter Kilewa, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya aliyeambatana na maafisa wengine watatu wa Jeshi Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kitengo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari wa Mkoa huo.