Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

TABOA: HATUVUTANI NA LATRA
Imewekwa: 04 May, 2023
TABOA: HATUVUTANI NA LATRA

Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimekanusha madai ya kuwepo kwa mvutano baina yake na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini siku ya Jumatano Mei 3, 2023.

Hayo yamesemwa na Bw. Priscus Joseph, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), wakati wa mkutano na wanahabari ulioandaliwa na LATRA kwa kushirikiana na TABOA uliofanyika katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Jumatano Mei 3, 2023.

Akizungumza na wanahabari Bw. Joseph amesema hakuna viashiria vyovyote vya kutokuelewana na LATRA kwani wamekuwa wakishirikiana katika mambo mbalimbali, huku wakishirikishwa katika kila jambo la maamuzi linalowahusu.

“Kumekuwa na sintofahamu kuwa kuna mvutano baina yetu na LATRA jambo ambalo sio kweli, sisi na LATRA tunashirikiana kwa kiasi kikubwa tofauti na inavyosemekana, tumeshirikiana katika mambo mengi kama upangaji wa nauli za mabasi, suala la Tiketi Mtandao tumekuwa tukiitwa ili tutoe maoni, kimsingi uongozi wa LATRA umekuwa ukitufikia kwa wakati,” amesema Bw. Joseph.

Aidha, Bw. Joseph ameelezea hitaji la TABOA kwa taasisi za serikali kama vile Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Jeshi la Polisi kuendelea kuwawekea mazingira rafiki ili kuboresha sekta ya Usafiri nchini.

“Ombi langu kwa TAMISEMI na Jeshi la Polisi watuboreshee zaidi stendi zetu na hali ya usalama ili dira yetu ya kusafiri saa 24 iweze kufikiwa kwa haraka,” amesema Bw. Joseph.

Kwa upande wake Bw. Salum Pazzy, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka LATRA, ameeleza kuwa ili kufanya kazi zake kwa ufanisi LATRA imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ambao moja kwa moja wanahusika na sekta ya usafiri ardhini.

“Napenda kuwashukuru wadau mbalimbali ambao tumekuwa tukishirikiana nao tunapofanya kazi zetu za udhibiti, wakiwemo Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na TABOA. Wadau kama TABOA ndio wanaotegemewa na Serikali ili kutoa huduma maana Serikali haina mabasi na wala haifanyi biashara, hivyo nawashukuru kwa kushirikiana katika mambo kama uanzishwaji wa Tiketi Mtandao,” amesema Bw. Pazzy.

Vilevile ameeleza kuwa Mamlaka ilianza majaribio ya safari za usiku kwa kuanza na safari za alfajiri mnamo Disemba 2022 ambapo kwanzia Mei mwaka huu Mamlaka imeanza kutoa ratiba kwa safari za mabasi kuanzia saa 9 usiku.

“Baada ya hoja zilizotolewa na waheshimiwa Wabunge, pamoja na kupokea maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Mhe. Mha. Hamad Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama kikosi cha Usalama Barabarani na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Mamlaka ilifanya majaribio ya safari za usiku kwa kuanza na safari za alfajiri mnamo Disemba 2022, zaidi ya mabasi 180 sasa yamepatiwa ratiba ya kusafiri kwanzia alfajiri, na mpaka Mei 1, 2023 Mamlaka imeanza kutoa ratiba kwa mabasi yenye uhitaji wa kuanza safari kwanzia saa 9 usiku” ameeleza Bw. Pazzy.

LATRA imekuwa ikifanya Mikutano na wadau mbalimbali ili kuweza kuboresha hali ya usafirishaji nchini, Mamlaka imekuwa ikiwaita wadau mbalimbali na kupokea maoni ili kuona namna bora ya kuboresha sekta ya usafiri, mikutano ya kujadili mambo kama nauli za mabasi, matumizi ya tiketi mtandao na nauli za daladala iliitishwa, wadau wakafika na kutoa maoi yao ambayo yalifanyiwa kazi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo