Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KAMATI YA URATIBU USAFIRI ARDHINI YAKAGUA MRADI WA SGR
Imewekwa: 18 May, 2022
KAMATI YA URATIBU USAFIRI ARDHINI YAKAGUA  MRADI WA SGR

Na. Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) tarehe 17 Mei, 2022 imewezesha ziara ya wajumbe wa Kamati ya Uratibu Usalama wa Usafiri Ardhini iliyotembelea na kukagua Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika kituo cha Dar es Salaam, Pugu, Soga na Karakana iliyopo Soga.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo,  Bw. Geofrey Silanda, Meneja Uratibu Usalama na Mazingira - LATRA ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo emesema kuwa Kamati imefanya ziara hiyo ili kuweza kukagua Maendeleo ya Mradi.

Aidha, Bw. Silanda amesema LATRA ina jukumu la kuratibu usalama wa usafiri ardhini na hivyo ziara hiyo inatekeleza moja ya majukumu ya Mamlaka.

'Kamati hii inakutana kila mwezi aidha, inaweza kukutana pale ambapo kuna uhitaji wa kufanya hivyo na pia inaainisha na kutatua kwa pamoja changamoto zilizowasilishwa na taasisi mbalimbali na lengo kubwa ni kuhakikisha kunakuwa na usalama katika usafiri ardhini", ameeleza Bw. Silanda 

Naye Mhandisi Thadei Paul, Meneja Mradi Msaidizi  SGR kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro kutoka katika Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema hadi sasa kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro kimefikia asilimia 96, kipande cha Morogoro mpaka Makutupora kimefikia zaidi ya asilimia 86, Makutupora mpaka Tabora ujenzi umeanza, kipande cha Tabora mpaka Isaka kipo kwenye hatua za mwisho  za kumpata mkandarasi na kipande cha Isaka mpaka Mwanza kimefikia zaidi ya asilimia 6.

Mhandisi Paul ameongeza kuwa, SGR itakuwa inatumia umeme na itatembea kwa kasi ya kilometa  160 kwa saa kwa treni ya abiria, na kilometa 120 kwa saa kwa treni ya mizigo na treni ya mizigo inatarajiwa kubeba tani milioni 17 kwa mwaka.

"Siku za hivi karibuni tumeanza majaribio ya treni na pia tulishaanza majaribio ya kuwasha umeme kwenye njia za treni. Mpaka sasa tumeshakagua  na umeme upo na majaribio yanaendelea", amefafanua Bw. Paul.

Naye Bi. Aisha Kabange, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) amesema kuwa kamati imefanya ukaguzi na wameona TRC imezingatia suala la usalama na pia amefurahishwa na hatua nzuri zilizochukuliwa za kuweka alama na njia maalum zitakazotumika na watu wenye mahitaji maalum, na hivyo mradi huu haujaacha mtu yeyote.

Naye Inspekta Abdallah Urutu kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ameipongeza Serikali kwa kuusimamia mradi huo na amesema miundombinu ya Zimamoto na Uokoaji imezingatiwa na mifumo thabiti na ya Kisasa imewekwa kwenye vituo vya SGR " Asilimia 99 ya mambo ya msingi ya Zimamoto na Uokoaji yamekamilika, hili ni jambo zuri sana".

Kamati hiyo inahusisha wajumbe wa taasisi mbalimbali zikiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Reli Tanzania na ZAMBIA (TAZARA), Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishatia na Maji (EWURA), Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Kikosi cha Reli ya Kati, TAZARA na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo