Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WADAU WAPONGEZA RASIMU ZA KANUNI MPYA ZA LATRA
Imewekwa: 23 Dec, 2024
WADAU WAPONGEZA RASIMU ZA KANUNI MPYA ZA LATRA

Wadau mbalimbali wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kufuatia uwasilishaji wa rasimu za Kanuni za LATRA za mwaka 2024 ambazo zinaenda kuwa mwarobaini wa changamoto za kiudhibiti wa sekta ndogo ya barabara, reli na waya.

Pongezi hizo zimetolewa Desemba 23, 2024 Ukumbi wa Mikutano Karimjee Dar es Salaam ulipofanyika Mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu rasimu za Kanuni za LATRA za mwaka 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Bw. Andrew Magombana Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Barabara, Wizara ya Uchukuzi aliyemuwakilisha  Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara

Rasimu za Kanuni hizo ni, Kanuni za Leseni za Watoa Huduma kwa Njia ya Reli za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2024, zilizolenga kuwadhibiti watoa huduma za usafiri watakaotumia miundombinu ya reli iliyojengwa na Serikali ambapo zimeweka utaratibu wa kutoa, kuhuisha na kufuta vibali na leseni kwa watoa huduma za usafiri wa reli, Kanuni za Usafiri wa Waya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2024 zilizolenga kusimamia utaratibu wa kutoa vibali na leseni kwa ajili ya udhibiti wa usafiri wa waya na Kanuni za Leseni Maalum za Sheria ya Utoaji wa Leseni za Usafirishaji za mwaka 2024 zilizolenga kuweka utaratibu wa kutoa, kuhuisha na kufuta leseni maalumu kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri wa umma.

Bi Catherine Lowi ni Mkurugenzi wa Nem Camp iliyopo chini ya Kampuni ya usafirishaji wa watali Ritungu ameeleza kuwa, Kanuni za usafiri wa waya zimekuja wakati sahihi kwa kuwa walikuwa wanapata changamoto za uendeshaji wa usafiri huo na pia Kanuni ni rafiki, zipo wazi na zinatenda haki kwa watoa huduma na wawekezaji kwa jumla.

“usafirishaji wa waya ni zao jipya ambalo linakuwa kwa kasi na watalii wanalifurahia na kwa jinsi Kanuni hizi zilivyo, tukizitekeleza naona tutafika mbali kwa wawekezaji wa ndani na nje na tunaona zinaenda kukuza sekta ya usafiri wa waya nchini,” amesisitiza Bi. Catherine.

Naye Bw. Fredrick Masawe, Afisa idara ya Biashara na Maendeleo Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema Kanuni hizo zitaongeza tija na chachu katika maendeleo ya usafiri wa reli nchini pia zitaweza kuwadhibiti watoa huduma wa sekta binafsi kutoa huduma katika njia ya reli.

Kwa upande wake Bw. Daudi Daudi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini amesema kuwa, “Tunachokitamani ni kuwa na kipengele cha mtoa huduma kutoa mkataba kwa watumiaji huduma ambao utambana mtoa huduma kutoa vigezo katika huduma atakayoitoa na hii itasaidia kuboresha huduma za usafiri nchini” amesema Bw. Daudi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, Bw. Andrew Magombana Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Barabara, Wizara ya Uchukuzi amesema, Kanuni hizo zimetokana na maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya sita hasa kwenye ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na barabara.

Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA ameeleza kuwa, Mamlaka inajukumu la kuhakikisha huduma zinakuwa bora nchini, “Sisi kama wadhibiti kwenye usafiri wa umma, usafiri wa mizigo na usafiri wa waya tunajukumu la kuhakikisha huduma hizi zinakuwa bora, salama, rafiki na za uhakika na katika utendaji wetu nyenzo za udhibiti ni Sheria, Kanuni na Taratibu na kinachofanyika leo ni kuhakikisha Kanuni hizo zinajadiliwa na kupokea maoni ya wadau ili tuweze kuziboresha,” ameeleza CPA Suluo.

Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na LATRA wanaendelea kupokea maoni ya maandishi kupitia baruapepe group.maoni@latra.go.tz  hadi tarehe 07 Januari, 2025.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo