Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WASAFIRISHAJI NA MADEREVA WAASWA KUZINGATIA SHERIA
Imewekwa: 04 Jan, 2025
WASAFIRISHAJI NA MADEREVA WAASWA KUZINGATIA SHERIA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa rai kwa madereva na wamiliki wa mabasi kutii Sheria ya leseni za usafirishaji ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi na kuepuka ajali zinazogharimu uhai wa watanzania.

Hayo yamebainishwa na Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA Januari 3, 2025 alipotoa tathmini fupi ya ukaguzi na udhibiti wa huduma za usafiri ardhini kipindi cha sikuku za mwisho wa mwaka 2024.

Bw. Pazzy amesema, LATRA imebaini changamoto za ukiukwaji wa masharti ya leseni za usafirishaji kwa mabasi maalum ya kukodi maarufu kama Special hire ambapo baadhi yao yanabeba abiria mmoja mmoja wa kuokoteza na kukiuka sharti la leseni la kusubiri kukodiwa wakisingizia uhitaji mkubwa wa huduma kwa wakati huo, na pia wengine wanakiuka matumizi sahihi ya Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i- Button).

Aidha ameeleza kuwa, kwa sasa Mamlaka kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wanafanya ukaguzi maalumu katika vituo mbalimbali vya maeneo ya kimkakati na endapo watabaini uvunjifu wa Sheria, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

“Tumeanzisha kampeni maalum ya kutoa elimu na kuhakikisha mabasi haya yanafungwa Kifaa cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD) na wanatumia kwa usahihi kitufe cha utambuzi wa dereva (i- Button) ili wakati wowote tuwatambue madereva wakiwa safarini. Pia, maafisa wetu wakishirikiana na mafundi wa VTD na Jeshi la Polisi wanafanya ukaguzi kwenye magari hayo,” amesema Bw. Pazzy.

Akitoa tathmini upande wa usafiri kwa njia ya reli, Bw Pazzy ameeleza kuwa huduma za usafiri wa treni ni nzuri ambapo usafiri wa treni ya kisasa (SGR) umerahisisha safari kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma na kurudi kupitia Morogoro na reli ya kati imekuwa na usafiri wa treni hadi mara tatu kwa wiki kuelekea mikoa ya Moshi na Arusha.

Vilevile amesema, Mamlaka imeendelea kudhibiti na kutoa leseni maeneo yenye uhitaji zaidi ili kurahisisiha huduma za usafiri kwa watanzania na pia amewasihi kutumia Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS)  https://pis.latra.go.tz/ kutambua mwendokasi wa basi na kutolea taarifa ya mabasi yanayotembea mwendo hatarishi kwa kupiga bure bila malipo siku zote kupitia namba 0800110019 au 0800110020.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo