Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, tarehe 30 Agosti, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda Wizara ya Uchukuzi baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Tangu kuundwa kwake, Wizara ya Uchukuzi imeendelea kutekeleza kazi zake kulingana na Hati ya Mgawanyo wa Majukumu iliyotolewa. Kwa heshima kubwa, ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Uchukuzi. Ninaomba kumhakikishia Mhe. Rais na Bunge lako Tukufu kuwa nitaendelea kutekeleza majukumu yangu kwa uaminifu mkubwa ili kuliletea Taifa letu maendeleo. Kwa muktadha huo, naomba kutoa Hotuba yangu ya kwanza ya Wizara ya Uchukuzi ambayo imejikita katika masuala ya usimamizi na uwezeshaji wa maendeleo ya miundombinu, huduma za uchukuzi na hali ya hewa kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa Wananchi. Aidha, napenda kumpongeza Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi baada ya iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kugawanywa.
Imewekwa: 06 May, 2024