Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imerejesha ratiba za mabasi tisa (9) ya Kampuni ya Ally’s Star yenye namba za usajili T946EBF, T947EBF, T948EBF, T354DXS, T357DXS, T360DXS, T233EBG, T232EBG na T178DVB na mabasi matatu (3) ya Kampuni ya Katarama Luxury yenye namba za usajili T835EBR, T836EBR na T212ECR. Basi la Ally’s Star litaanza safari saa tisa kamili (9:00) alfajiri na Katarama saa kumi kamili (10:00) alfajiri kuanzia Agosti 12, 2023 ili kuepusha mashindano yasiyo na tija kwa kukimbizana kuwahi kufika.
Hayo yamebainishwa na Bw. Salum Pazzy, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) alipozungumza na waandishi wa habari Agosti 11, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
“Mamlaka imekua ikifuatilia utoaji wa huduma za wasafirishaji hawa kwa ukaribu kupitia wataalam wetu nchi nzima ikiwa ni pamoja na uzingatiaji wa ratiba yaani muda wa kuanza safari, utumaji wa taarifa katika mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari, mwendokasi wa mabasi na matumizi ya kitufe cha utambuzi wa dereva (I-Button). Baada ya kuona kuwa wamejirekebisha ndio tumeamua kuwarejeshea ratiba hizo,”amesema Bw. Pazzy.
Vilevile amesema kuwa, LATRA imekua ikitoa elimu kwa wafanyakazi na wamiliki wa kampuni hizo ikiwa ni pamoja na matumizi ya Mfumo wa kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) pamoja na kufanya vikao vya pamoja na wamiliki wa makampuni hayo ambapo wametoa ahadi ya kuongeza ufuatiliaji wa mabasi yao.
Aidha, Bw. Pazzy ameeleza kuwa, uamuzi huo ni kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) (b) na 6(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413 na Kanuni za Leseni za Usafirishaji Magari ya Abiria za Mwaka 2020 ambapo pamoja na mambo mengine, LATRA ina jukumu la kutoa, kuhuisha na kufuta vibali na leseni za usafirishaji, na kukuza usalama wa sekta zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na usalama wa watumiaji wa huduma.
Naye Bw. Abdallah Maulid Abdallah, Mtendaji Mkuu kutoka basi la Ally’s Star na Bw. Elimboto Njoka Mtatuu, Meneja Uendeshaji Kutoka Katarama Luxury wamemshukuru CPA Habibu Suluo na Uongozi wa LATRA kwa ushirikiano walioonesha na wameahidi kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani ili kuwa na usafiri ardhini ulio bora na salama.
Ikumbukwe kuwa, tarehe 19 Juni, 2023 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilisitisha ratiba ya mabasi ya Ally’s Star na Katarama Luxury kuanza safari saa tisa (9:00) alfajiri na saa kumi na moja (11:00) alfajiri na kupewa ratiba ya kuanza safari saa kumi na mbili (12:00) asubuhi. Hatua hiyo ilitokana na Mamlaka kupata taarifa na kuthibitisha uwepo wa mabasi ya kampuni hizo yanayokwenda mikoani kuchezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na hivyo kusababisha kusafiri kwa mwendo kasi kwa lengo la kufanya mashindano ya kuwahi kufika kwenye vituo/stendi za mabasi.