Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb) Naibu Waziri wa Uchukuzi ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kutekeleza maelekezo ya kuandaa maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini yanayofanyika Novemba 24 hadi 29, 2025 Dar es Salaam.
Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo Novemba 24, 2025 alipofungua maonesho ya Maadhmisho ya kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini yanayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam na kuhusisha wadau wa usafirishaji wa ndani na nje ya nchi wanaotoa elimu na huduma kwa wananchi wanaotembelea viwanjani hapo.
“Tunawapongeza kwa kutekeleza agizo hili kwa ubunifu mkubwa na kupitia wiki hii, tutajifunza jinsi matumizi ya nishati safi yanavyotunza mazingira na kupunguza gharama za usafirishaji na pia tutaona ubunifu wa mifumo ya sekta ya usafirishaji inavyorahisisisha utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Mhe. Kihenzile.
Vilevile ameipongeza LATRA kwa kazi nzuri ya udhibiti usafiri ardhini inayoifanya ambapo kwa sasa ushirikiano na wadau umeongezeka na mifumo ya kiudhibiti inafanya kazi ambayo inarahisisha utoaji wa huduma kwa wadau ambao ndio watumiaji wa huduma hizo.
Naye Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi LATRA ameishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa usimamizi wa karibu kwa LATRA uliochangia kufanikisha kwa ufanisi utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa.
Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini inaadhimishwa Novemba 24 hadi 29 Dar es Salaam na maadhimisho hayo yanafanyika sambamba na Siku ya Usafiri Endelevu Duniani inayoadhimishwa Novemba 26 kila mwaka. Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 ni Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji.

