Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

BODI YA WAKURUGENZI NA MENEJIMENTI YA LATRA WAPIGWA MSASA AFYA YA AKILI
Imewekwa: 28 Jul, 2023
BODI YA WAKURUGENZI NA MENEJIMENTI YA LATRA WAPIGWA MSASA AFYA YA AKILI

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Menejimenti wametakiwa kuzingatia Afya zao ikiwemo Afya ya Akili ili kutoathiri utendaji kazi wao wawapo kazini.

Hayo yamesemwa na Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA, Jijini Dar es Salaam katika semina maalum iliyoandaliwa na LATRA kwa ajili ya Wajumbe wa Bodi ya LATRA na Menejimenti ili kupatiwa elimu ya Afya ya Akili iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa ofisi ya LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, Julai 27, 2023.

Akizungumza na wajumbe wa Semina hiyo, Prof. Ame amewasisitiza kujitambua wakiwa katika hali ya msongo wa mawazo na kutafuta msaada wa kitaalamu kama ilivyoshauriwa na Mkufunzi wa Semina hiyo Dkt. Garvin Kweka, kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Binafsi najijua, kama nikiona tabia yangu ya ulaji imebadilika, mathalan hamu ya kula kuongezeka basi najua kuwa nina shida, haraka namuona daktari. Hivyo niwasihi tuu kama alivyoshauri daktari ukiona hauko sawa iwe ni msongo wa mawazo au shida nyingine ambayo inaweza kuathiri utendaji kazi wako muone mtaalamu ili upate msaada,” amesema Prof. Ame.

Kwa upande wake Dkt. Garvin Kweka, mkufunzi wa semina hiyo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati akiendelea na mafunzo hayo amesema kuwa vipo viashiria mbalimbali ambavyo vinawezea kusaidia kutambua kuwa mtu binafsi hauko sawa au jirani yako hayuko sawa, na hii itasaidia kuepusha athari zinazoweza kusababishwa na matatizo kwenye afya ya akili.

“Yapo mambo mengi ambayo yanaweza kukuonesha kuwa hauko sawa, au mtu mwingine hayuko sawa, kiashiria kikubwa ni mabadiliko ya tabia kwa ghafla, mathalan mtu huwa ni mcheshi sana lakini anakuwa mkimya ghafla, hii inaashiria kuna kitu kinamsumbua, sasa kwa kulijua hilo mnaweza kuchukua hatua za ziada ili kumsaidia kuwa sawa hivyo kupunguza uwezekano wa kuchukua hatua za kujidhuru,” amesema Dkt. Kweka.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Afya ya Akili ni ile hali ambapo akili ya mtu inaweza kuhimili hali ya maisha inayoweza kuleta msongo wa mawazo, kutumia vyema uwezo wake, kufanaya kazi na kujifunza vizuri na kumfanya mtu kuishi vizuri kutokana na misingi ya jamii yake. Hii hutambuliwa na namna mtu anaweza kuitikia hisia zake.

Afya ya Akili isipokuwa sawa inaweza kusababisha msongo wa mawazo ambao unaweza kuleta athari mbalimbali kama vile migogoro ya kifamilia, kupungua kwa ufanisi katika shughuli mbalimbali, matumizi ya mihadarati, matatizo ya uhusiano na hata kutengwa na jamii, na matokeo yake yanaweza kusababisha mtu kujidhuru, hivyo ni vyema kila mmoja kutilia mkazo suala la Afya ya Akili ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na uzalishaji unakuwa endelevu.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo