Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewasihi wadau wa sekta ya usafiri ardhini nchini kuimarisha ushirikiano na kutumia majadiliano ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea kuwa salama, nafuu na za uhakika kwa watanzania.
Hayo yameelezwa na CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA wakati wa semina ya mafunzo kwa wandishi wa habari mabalozi wa LATRA iliyofanyika Aprili 1 na 2, 2026, ukumbi wa mikutano wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere uliopo Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa, sekta binafsi ina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za usafiri na ukuaji wa uchumi wa Taifa, hivyo ushirikiano wao na Serikali ni nguzo muhimu katika kuijenga sekta imara na endelevu.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wadau wa sekta binafsi katika kutoa huduma za usafiri na kuchochea maendeleo ya uchumi. Ushirikiano wenu na Serikali ni muhimu ili kuhakikisha sekta hii inaendelea kukua na kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema CPA, Dkt. Suluo.
Amesisitiza kuwa pindi changamoto za huduma za usafiri na usafirishaji zinapojitokeza, ni busara wadau kukaa pamoja na Mamlaka kwa majadiliano ya kina, wazi, na ya kujenga ili kufikia suluhu ya pamoja, badala ya kuchukua hatua za ghafla mathalan kusimamisha huduma au kupandisha nauli bila kufuata taratibu zilizowekwa hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko ya gharama za uendeshaji kama vile bei za mafuta jambo ambalo linaathiri watanzania na uchumi kwa jumla.
Wakati huohuo CPA Dkt. Suluo amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uweledi, uadilifu na uzingatiaji wa maadili ya taaluma yao, akibainisha kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kuwafikishia kuhakikisha taarifa sahihi kwa wakati.
Ameongeza kuwa, LATRA itaendelea kuwajengea uwezo wanahabari kupitia mafunzo na ushirikiano wa karibu ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa zinazohusu udhibiti na maendeleo ya sekta ya usafiri ardhini nchini.
Mafanikio ya sekta ya uchukuzi yanategemea ushirikiano na uwajibikaji wa wadau wote ili kujenga sekta iliyo salama, thabiti na yenye manufaa kwa watanzania wote.

