CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema kuwa, nauli za usafiri wa umma kwa njia ya barabara hazipangwi kwa kuzingatia bei ya mafuta peke yake bali uwekezaji mzima uliofanyika.
CPA, Dkt. Suluo amebainisha hayo kwenye mkutano wa wadau kuhusu mchakato wa mapitio ya nauli za usafiri wa umma kwa njia ya barabara uliofanyika Aprili 8, 2026 ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa, Kanuni za Tozo za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za mwaka 2020 (GN Na. 82 ya tarehe 7/2/2020) zinaelekeza utaratibu wa Mtoa Huduma kuwasilisha mapendekezo ya mapitio ya nauli au Mamlaka kuanzisha mchakato pale inapobidi, ili kuhakikisha kuwa nauli zinaakisi gharama halisi za uendeshaji na kulinda uendelevu wa huduma za usafiri wa umma.
“Leo tumekutana na wadau wa usafiri ardhini ili kupata maoni yao kuhusu hatua za kuchukuliwa endapo gharama za mafuta zitaendelea kuongezeka. Maoni yao ni muhimu sana kwa kuwa yataisaidia Mamlaka katika kufanya mapitio ya nauli za huduma za usafiri wa umma kwa njia ya barabara “ amesema CPA, Dkt. Suluo.
Ameongeza kuwa, Sheria ya LATRA Sura ya 413, inaelekeza kuwa nauli zinaweza kufanyiwa mapitio kwa angalau kila baada ya miaka mitatu labda itokee mtoa huduma aseme kuwa mrejesho wa uwekezaji wake ni chini ya asilimia 10 au watumiaji wa huduma waseme msafirishaji anapata zaidi ya asilimia 25.
“Kwa hesabu zetu, takwimu tulizonazo na kwa kikokotoo chetu tunaona bei ya mafuta ya sasa haiathiri nauli labda bei izidi na huu ni mwezi wa 29 tangu Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA) itangaze bei ya mafuta Desemba 6, 2023 na sisi nauli zetu zilianza Desemba 2023. Ndani ya Serikali kuna jitihada zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha bei hazipandi tena na ikiwezekana zishuke bila kuathiri maeneo mengine.,” ameeleza CPA, Dkt. Suluo.
Mkutano huo umehudhuriwa na wadau wa usafiri ardhini kutoka vyama vya wasafirishaji, watumiaji wa huduma za usafiri, Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) pamoja na viongozi wa LATRA. Wadau hao walifanya mawasilisho yao kuhusu marejeo ya nauli na kwa wale walioshindwa kushiriki wanaweza kuwasilisha maoni yao ndani ya siku 14 hadi tarehe 22 Aprili, 2026 kwa baruapepe info@latra.go.tz

