Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA, DKT. SULUO: USHIRIKISHWAJI WA WADAU NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI
Imewekwa: 30 Jan, 2026
CPA, DKT. SULUO: USHIRIKISHWAJI WA WADAU NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Dkt. Habibu Suluo, amesema ushirikishwaji wa wadau ni nguzo muhimu katika kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini, hatua inayoongeza ufanisi, tija na kusaidia watoa huduma kutii sheria bila shuruti.  

CPA, Dkt. Suluo amebainisha hayo Januari 19, 2026, katika kipindi cha dakika 45 kilichofanyika katika kituo cha habari cha ITV, ambapo ameeleza kuwa LATRA ina taratibu maalum za kuwashirikisha wadau wa sekta ya usafirishaji kabla ya kufanya mabadiliko yoyote katika utoaji wa huduma kwenye njia mbalimbali.

“Kabla ya kuwaondoa watoa huduma katika njia fulani au kuwasitishia leseni, hususan watoa huduma za usafiri wa daladala, ni lazima Mamlaka iwape mbinu mbadala na kuwaeleza mwelekeo wa mabadiliko yanayokusudiwa, mabadiliko ni mchakato unaohitaji maelewano na ushirikishwaji wa wadau ili kuhakikisha yanakubalika na kutekelezwa kwa ufanisi,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Aidha, CPA, Dkt. Suluo amesema LATRA tayari imefanya vikao na Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA) pamoja na Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam (UWADAR), ambapo wamejadili na kukubaliana namna ya kuwapa fursa ya kushiriki katika ruti maalum, ikiwemo ruti ya Gongolamboto, kwa mfumo wa uwekezaji unaozingatia maslahi ya wawekezaji wadogo.

LATRA inaendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kushirikisha wadau, kurasimisha watoa huduma na kuboresha huduma za usafiri ardhini kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata usafiri salama, wa uhakika na wenye tija.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo