Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA SULUO: WATEJA NI KIPAUMBELE CHETU
Imewekwa: 10 Oct, 2025
CPA SULUO: WATEJA NI KIPAUMBELE CHETU

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema LATRA inathamini na inatambua mchango wa wateja katika kuboresha huduma na utendaji kazi wa Mamlaka na wao ndio kipaumbele cha Mamlaka hiyo.

CPA Suluo ameeleza hayo ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Oktoba 08, 2025 kwenye maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanayofanyika Oktoba 06 hadi 10, 2025 ambapo aliwahudumia wateja kikamilifu, kusikiliza maoni na kutatua changamoto za wateja waliotembelea ofisi hiyo.

“Wateja ni namba moja kwetu na sisi tupo kwa ajili ya kuwahudumia, endapo hawajaridhika na huduma za Mamlaka wawasilishe maoni au malalamiko yao kwa namba bila malipo 0800110019 au 0800110020 au kupitia mfumo wa eMrejesho, pia wawasilishe video za ushahidi wa vitendo vyote vinavyofanyika kwenye usafiri wa umma ambavyo vinavunja Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini nasi tutapokea na kufanyia kazi”, amesema CPA Suluo.

Vilevile amebainisha kuwa, Mamlaka imebuni na kutengeneza mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji kazi wa Mamlaka na utoaji wa huduma za usafiri ardhini nchini.

“Wateja wetu wanaweza kuomba, kupata na kuhuisha leseni za usafirishaji kwa mtandao kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Reli na Barabara (RRIMS) rrims.latra.go.tz/, wanaweza kukata tiketi za Treni na Mabasi kwa mfumo wa Safari Tiketi tiketi.latra.go.tz/  kufahamu nauli halali za magari ya mijini (daladala) na mabasi yanayoenda mkoani kwa kupakua LATRA APP inayopatikana Play Store. Pia kwa sasa vituo vya mabasi vipo kiganjani kupitia Mfumo wa Taarifa kwa Abiria pis.latra.go.tz/,” ameeleza CPA Suluo.

Kaulimbiu ya Wiki ya Huduma kwa Wateja ni “Mission: Possible” yaani "Mipango Imewezakana" ambapo mipango ya LATRA ya kuboresha huduma zake imewezekana kupitia mifumo ya TEHAMA pia imeweza kusogeza huduma zake karibu na wadau kupitia ofisi zake zinazopatikana kote Tanzania Bara.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo