Watoa huduma wa usafiri wa magari ya mjini (Daladala) wamekumbushwa kuzingatia masharti ya leseni za usafirishaji inayowataka kutoa huduma bora na salama ikiwemo kutokatisha ruti na kutozidisha nauli kwa abiria hali ambayo husababisha usumbufu kwa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini nchini.
Amesema hayo Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA Agosti 6, 2026 alipozungumza na Kituo cha Redio cha Malkia Choice jijini Dar es Salaam, ambapo alieleza kwa mujibu wa Sheria magari yote yanayotoa huduma ya safari za masafa marefu na magari ya usafiri wa mjini(daladala) yanatakiwa kufungwa Kifaa cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD) .
Amesema kuwa kwa sasa zoezi la kufunga VTD kwenye daladala limeanza kwa awamu, ambapo daladala zinazobainika kukiuka masharti ya leseni za usafirishaji zinafungwa kifaa hicho ili kuwezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa magari hayo na kudhibiti ukiukwaji wa masharti hayo usijirudie.
“Nawakumbusha wahudumu wa usafiri wa daladala, yaani madereva na makondakta kwamba, endapo daladala itabainika kufanya makosa ya kukatisha ruti au kutoza nauli kinyume na taratibu, pamoja na adhabu nyingine gari hilo halitaruhusiwa kuendelea kutoa huduma barabarani hadi litakapofungwa kifaa cha VTD”, amesema Bw. Pazzy.
Amefafanua kuwa kifaa hicho kitaiwezesha Mamlaka kufuatilia mwenendo wa gari, ikiwemo kujua linapoanzia safari, linapomalizia safari pamoja na mwendokasi wake, hivyo kusaidia kuimarisha udhibiti na utii wa masharti ya leseni.
Bw. Pazzy amesema kuwa zaidi ya daladala 201 zilizobainika kukiuka masharti ya leseni walizopewa zimefungiwa vifaa vya VTD, hatua ambayo imesaidia kuimarisha nidhamu ya magari hayo barabarani na kupunguza vitendo vya kukatisha ruti vinavyosababisha usumbufu kwa abiria.
Aidha, Bw. Pazzy amewakumbusha watoa huduma wenye leseni za magari maalum ya kukodi (Special Hire) kuwa, hawaruhusiwi kutumia magari hayo kutoa huduma za usafiri wa daladala. Leseni hizo zinawaruhusu kutoa huduma kwa vikundi maalum au abiria wanaosafiri pamoja katika safari moja, gari litakalobainika kutumika kinyume na masharti ya leseni litachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizowekwa.
LATRA imeendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa wanapobaini ukiukwaji wa Sheria, Kanuni au masharti ya leseni za usafirishaji kupitia namba za huduma kwa wateja 0800 110 019 na 0800 110 020, au kwa kurekodi na kutuma ushahidi wa tukio kupitia WhatsApp namba 0681 300 800 ili kuimarisha utii wa Sheria, kuboresha huduma za usafiri wa umma na kuhakikisha abiria wanapata huduma bora, salama na za uhakika.

