Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

DCP KAHATANO: TUSHIRIKIANE KUTOKOMEZA RUSHWA
Imewekwa: 29 May, 2025
DCP KAHATANO: TUSHIRIKIANE KUTOKOMEZA RUSHWA

DCP Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi wadau wa usafiri ardhini kushirikiana na LATRA katika jitihada za kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ili kuwa na sekta ya usafiri ardhini yenye tija.   

DCP Kahatano amebainisha hayo kwenye semina ya kukuza maadili na kupambana na rushwa iliyoandaliwa na Kamati ya Uadilifu ya LATRA kwa Taasisi zisizo za Kiserikali na kufanyika Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, Mei 29, 2025.

Katika semina hiyo, DCP Kahatano amesema kuwa, Mamlaka inakemea vikali vitendo vya rushwa na inatambua kuwa suala la kupambana na rushwa ni mtambuka hivyo ni muhimu kila mdau wa usafiri ardhini kutambua nafasi na wajibu wake kwa kukataa vitendo hivyo ambavyo vina athari kubwa katika utoaji wa huduma kwa watanzania.

“Tunatambua rushwa ni adui wa haki na ni matokeo ya ukiukwaji wa maadili,  hivyo endapo kutakuwa na viashiria vyovyote vya vitendo vya rushwa LATRA, tunaomba muwasiliane nasi kwa kupiga simu bila malipo  kwa namba 0800110019/20, kutumia mfumo wa emrejesho https://emrejesho.gov.go.tz/ , baruapepe ya Mamlaka kwa anwani ya info@latra.go.tz au kuwasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili hatua zichukuliwe kwa haraka.

Vilevile amesema, Serikali inatekeleza Mkakati wa Taifa dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelzaji Awamu ya Nne wa mwaka 2023 – 2030 wenye lengo mahususi la kushirikisha sekta binafsi kwenye mapambano dhidi ya rushwa na kukuza uadilifu.

Mhandisi Eliud Kataraihya, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) LATRA amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anasisitiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha mifumo hiyo inabadilishana taarifa ambapo LATRA inatekelza hilo kwa vitendo kwa kubuni na kutumia mifmo ya TEHAMA katika shughuli zake za kiudhibiti.

Ameongeza kuwa, Mamlaka inabuni na inatumia mifumo ya TEHAMA kutoa huduma kwa wadau wake ambapo kwa sasa wadau hao hawalazimiki kuonana na mtumishi wa Mamlaka pindi unapotaka kupata huduma, hali ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti vitendo vya rushwa, kuongeza uwazi na uwajibikaji.

“Kwa upande wa madereva wa vyombo vinavyodhibitiwa na LATRA, kuna Mfumo wa Kutahini Madereva yaani DTS ambapo dereva anapofanya mtihani wa kuthibitishwa na Mamlaka, Mfumo ndio unachagua maswali, kusahihisha na kutoa alama. Haya yote yanafanyika bila kuwa na mtu wa kati, kwa hiyo kwa mazingira haya, imesaidia kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo vinadidimiza haki ya mdau”, ameeleza Mha. Kataraihya.

Nae Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA amesema miongoni mwa jitihada zinazotekelezwa na LATRA za kupambana na rushwa ni kupitia utoaji wa elimu kwa umma kwa njia mbalimbali ikiwemo redio, runinga, mitandao ya kijamii, kushiriki kwenye maonesho pamoja na mikutano mbalimbali ya wadau.

Kwa upande wake,Bi. Marcella Salu, Afisa Mchunguzi Mkuu kutoka TAKUKURU amesema rushwa ni adui wa haki na kila mmoja anawajibika kupambana na vitendo vya rushwa na kuvitolea taarifa kwa Mamlaka husika kwa kuwa vitendo hivyo vina madhara mengi ikiwemo kukwamisha utoji wa haki, kuzorotesha mendeleo ya nchi, kutolewa kwa huduma duni au kukosekana kwa huduma, kudhoofisha nguvu kazi ya Taifa pamoja na kukosekana kwa amani na kuchochea chuki kwa wananchi.

Nao wadau waliohudhuria semina hiyo wameipongeza LATRA kwa kuwashirikisha katika masuala yanayohusu sekta ya usafiri ardhini na wameishukuru kwa kuwapatia elimu hiyo na wameahidi kuiwasilisha kwa wengine.

Semina hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSTOA), Umoja wa wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA), Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Usafirishaji (TADWU), Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (CHAWAMATA), Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) Pamoja na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC).

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo