Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. KWAGILWA AIPONGEZA LATRA UHAMASISHAJI MATUMIZI YA NISHATI SAFI
Imewekwa: 01 Jun, 2026
MHE. KWAGILWA AIPONGEZA LATRA UHAMASISHAJI MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Mhe. Reuben Nhamanilo Kwagilwa (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa juhudi za kuendelea kudhibiti sekta ya usafiri ardhini nchini huku ikizingatia uhifadhi wa mazingira kwenye vyombo vya usafiri sambamba na kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika magari ya abiria ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu.

Mhe. Kwagilwa ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la LATRA katika Maonesho ya Wiki ya Mazingira yanayofanyika Juni 01 hadi 05, 2026 viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma, ambapo alielezwa kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Mamlaka katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwenye huduma za usafiri wa magari ya abiria.

Mhe. Kwagilwa (Mb) amesema, LATRA imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira katika usafiri wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT), pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) na vyombo vingine vya usafiri kibiashara, hatua inayochangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda afya za wananchi.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kutafakari na kupitia utaratibu wa kupunguza baadhi ya tozo na ushuru kwa magari na bajaji zinazotumia nishati safi ili kuhamasisha uwekezaji mkubwa zaidi katika teknolojia hizo na kuongeza matumizi ya vyombo vya usafiri visivyochafua mazingira.

“Serikali inaona umuhimu wa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika sekta ya usafiri. Tutaangalia uwezekano wa kupunguza baadhi ya tozo na ushuru kwa magari na bajaji zinazotumia nishati safi ili kuvutia uwekezaji na kuongeza matumizi ya teknolojia hizi rafiki kwa mazingira,” amesema Mhe. Kwagilwa.

Kwa upande wake Bw. Augustus Fungo, Afisa Huduma kwa Wateja Mkuu LATRA, amesema Mamlaka inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia ustawi wa Watanzania na umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Vilevile amesema, LATRA inatekeleza kwa vitendo Uendelevu wa Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG) pamoja na kuimarisha shughuli za Idara ya Usalama na Mazingira ili kuhakikisha huduma za usafiri zinatolewa kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi wa mazingira.

Pia, amesema Mamlaka inaendelea kuhimiza matumizi ya tiketi za kielektroni ili kupunguza matumizi ya karatasi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za usafiri wa umma.

Aidha, amesema LATRA inaendelea kuwahimiza watoa huduma za usafiri ardhini kuhakikisha mabasi yanasimama kwenye vituo na maeneo yaliyoidhinishwa ili kuwawezesha abiria kupata huduma za kijamii. Pia, LATRA inaendelea kuhamasisha uwepo na matumizi sahihi ya vyombo vya kuhifadhia taka ndani ya vyombo vya usafiri na maeneo ya huduma ili kudumisha usafi na kulinda mazingira.

LATRA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia na nishati safi katika sekta ya usafiri ardhini, sambamba na kuhakikisha huduma za usafiri zinakuwa salama, bora na rafiki kwa mazingira.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor