Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA, DKT. SULUO: TUNATHAMINI KALAMU ZENU
Imewekwa: 22 Apr, 2026
CPA, DKT. SULUO: TUNATHAMINI KALAMU ZENU

CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amesema kuwa Serikali kupitia LATRA inatambua na inathamini kazi kubwa inayotekelezwa na wanahabari nchi ya kuelimisha umma kuhusu jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi kupitia sekta ya usafiri na usafirishaji nchini.

Amesema hayo wakati wa semina ya mafunzo kwa wanahabari mabalozi wa LATRA iliyofanyika tarehe 1 na 2 Aprili, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, Mkoa wa Pwani ili kuwajengea uwezo na kuimarisha ushirikiano.

“Wanahabari ni kiungo muhimu sana kati ya wananchi na Serikali yao, tunathamini kalamu zenu kwa kuwa zina athari kubwa ikiwemo kuchochea maendeleo ya nchi lakini ikitumika vibaya inaweza kuvuruga amani na mshikamano tulionao kama nchi, hivyo ni vyema mkazitumie kwa manufaa ili kuendelea kujenga amani, utulivu na uzalendo kwa watanzania wote,” amesema CPA, Dkt. Suluo,

Vilevile amesema, LATRA imejiwekea utaratibu wa kukutana na wanahabari mabalozi wao kila mwaka ili kuzungumza kuhusu mafanikio ya sekta ya usafiri ardhini, changamoto zilizopo, jitihada za kuzitatua pamoja na mwelekeo wa Mamlaka wa kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji nchini kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Pia, CPA, Dkt. Suluo amesema kuwa, Mamlaka inajivunia kuwa na mabalozi wanahabari hao ambao wamekuwa mstari wa mbele kutoa mrejesho na kuwasilisha maoni mbalimbali ya maeneo ya kuyafanyia maboresho pale ambapo kunatokea changamoto ili wananchi waweze kuridhika na huduma za zinazotolewa na LATRA.

Aidha, Dkt. Suluo amesema kuwa, LATRA inatekeleza majukumu yake kwa niaba ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyechagiza mafanikio ya Mamlaka hiyo ambapo matunda ya uongozi wake mahiri yanajidhihirisha kwa kuacha tabasamu kwa wananchi wake.

“Tumekuwa tukitekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia falsafa nne za Mhe. Rais ambazo ndio zinatuongoza katika kupata mafanikio haya mnayoyaona ikiwemo kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, kushirikiana vizuri na wadau wetu, kutengeneza na kutumia mifumo inayoboresha upatikanaji wa huduma za usafiri ardhini mathalan mfumo wa Safari Tiketi ambapo kwa sasa mwananchi ana uwezo wa kukata tiketi wakati wowote na mahali popote alipo bila kulazimika kufika kituo cha mabasi.

Kwa upande wake Bi. Rukia Kibwana, Afisa Mfawidhi wa LATRA Kituo cha Mabasi Magufuli, amesema semina hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa imewapa wanahabari fursa ya kubadilishana uzoefu na kuongeza uelewa kuhusu sekta ya usafiri wa barabara.

Pia Bi. Rukia ameeleza kuwa wanahabari hao wamepata uelewa kuhusu huduma za LATRA zinazotolewa saa 24 pamoja na Kituo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kilichopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam, ambazo husaidia kushughulikia changamoto za usafiri wakati wote.

Naye Bw. Paul James, mwanahabari balozi wa LATRA amebainisha kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini na itakuwa rahisi kwao kutumia elimu hiyo wanapotekeleza majukumu yao ya kuhabarisha umma.

“Mafunzo tuliyopata ni muhimu sana na yasingeweza kumfikia mtu mmoja mmoja kwa urahisi, hivyo yatawafikia kupitia vyombo vya habari. Mafunzo haya yametukumbusha umuhimu wa kuelewa Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini ili tuweze kuhabarisha umma kwa usahihi,” amesema Bw. James.

LATRA inaendelea kujivunia ushirikiano wake na wanahabari mabalozi ambao wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika kuhabarisha umma kuhusu masuala ya usafiri na usafirishaji kwa sekta ya usafiri ardhini nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo