Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAGEUZI YA KIDIGITI: PROF. KAHYARARA APONGEZA UBUNIFU NA UTENDAJI WA LATRA MAONESHO YA SABASABA
Imewekwa: 03 Jul, 2026
MAGEUZI YA KIDIGITI: PROF. KAHYARARA APONGEZA UBUNIFU NA UTENDAJI WA LATRA MAONESHO YA SABASABA

Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa mapinduzi makubwa ya uboreshaji wa huduma kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayowezesha upatikanaji wa huduma kwa urahisi, uwazi na wakati.

Prof. Kahyarara ameyasema hayo alipotembelea jengo la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), mtaa wa mazao katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Julai 1, 2026, ambapo alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka pamoja na maboresho ya mifumo ya kidigiti inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Vilevile amesema LATRA imekuwa ikitekeleza kwa vitendo maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kubuni, kusanifu na kutumia mifumo ya TEHAMA katika shughuli za kiudhibiti hatua ambayo imeongeza ufanisi na tija katika sekta ya usafiri ardhini nchini.

Pia, Prof Kahyarara ameipa kongole LATRA kwa kuwa karibu na wadau na kuwashirikisha katika uamuzi wa kiutendaji jambo linaloongeza umoja, mshikamano na hatimaye kuimarisha sekta pasi na kuwa na migogoro isiyo na lazima kati ya wasafirishaji na mdhibiti.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya, najua ni ngumu na bahati nzuri naona sasa mnaeleweka na wadau wetu, mapinduzi makubwa yamefanyika katika mageuzi ya mifumo, niwakaribishe wote wanaotembelea maonesho haya ya Sabasaba wasiache kutembelea jengo la LATRA ili kujifunza matumizi ya mifumo hii,” amesema Prof. Kahyarara.

Kwa upande wake Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, amemueleza Prof. Kahyarara kuwa, Mamlaka imejizatiti kuhakikisha wasafirishaji wanatoa huduma bora, salama na zenye staha huku wakitii Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini zilizopo.

“Kama ilivyo kaulimbiu yetu ‘Pamoja kwa Usafiri Bora’, kama Mamlaka tunajitahidi kuhakikisha kuwa kwa kushirikiana na wadau wetu tunafanya huduma za usafiri nchini zinazidi kuimarika, kupitia mifumo ya kisasa iliyorahisishwa na kusikilizana,” amesema Bw. Pazzy

LATRA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea jengo lake katika Maonesho ya Sabasaba 2026, kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo mifumo inayotumiwa katika udhibiti kama vile mfumo wa Safari Tiketi, elimu ya utunzaji mazingira kupitia matumizi ya nishati safi.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor