Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

DKT. MSONDE: MIFUMO YENU IMEPUNGUZA MIANYA YA RUSHWA
Imewekwa: 07 Aug, 2026
DKT. MSONDE: MIFUMO YENU IMEPUNGUZA MIANYA YA RUSHWA

Dkt. Charles Msonde, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kubuni na kutumia mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), akieleza kuwa imeongeza ufanisi wa utendaji kazi, imeboresha utoaji wa huduma kwa wadau wa sekta ya usafiri ardhini na imechangia kupunguza mianya ya rushwa kupitia utoaji wa huduma kimtandao.

Pongezi hizo amezitoa alipotembelea banda la LATRA kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane Agosti 5, 2026 viwanja vya John Malecela jijini Dodoma kwa kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050” ambapo alielezwa kuhusu Mfumo wa Safari Tiketi (CeTS), Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS), Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo Tumizi wa LATRA App na Mfumo wa e-Mrejesho inavyofanya kazi kwa ufanisi.

Dkt. Msonde amesema matumizi ya mifumo ya kidigiti yamekuwa nguzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi sambamba na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya usafiri ardhini.

"Nawapongeza LATRA kwa kufanya kazi kubwa ya kuboresha huduma kupitia mifumo ya TEHAMA katika shughuli zenu za kila siku. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, dunia ya sasa haihitaji tena kufanya kazi kwa kutumia makaratasi ambayo si rafiki kwa mazingira, bali kutumia mifumo ya kidigiti inayorahisisha utoaji wa huduma na kuyahifadhi mazingira," amesema Dkt. Msonde.

Ameongeza kuwa, matumizi ya mifumo ya kidigiti yanasaidia kudhibiti vitendo vya rushwa kwa kuwa huduma nyingi kimtandao bila kuhitaji mawasiliano ya ana kwa ana kati ya mteja na mtoa huduma.

"Msafirishaji anayehitaji leseni ya chombo cha moto kibiashara anaweza kufanya maombi kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Reli na Barabara (RRIMS), ambapo hatua zote za uchakataji wa maombi hufanyika kimtandao hadi leseni inapopatikana, mfumo huu unapunguza mianya ya rushwa, unaongeza uwazi na unaharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi," ameeleza Dkt. Msonde.

Pia ametoa kongole kwa LATRA kwa kutengeneza Mfumo wa Safari Tiketi unaopatikana kwa njia ya tovuti https://tiketi.latra.go.tz/passenger/home au kwa kupakua kwenye simu janja ambao ni lango la tiketi za treni na mabasi na ameisihi Mamlaka kuendelea kuwahimiza watoa huduma wote kutoa tiketi za kielektroni kwa kila abiria ili wananchi waendelee kunufaika na manufaa ya mfumo huo kwa kukata tiketi halali zenye nauli elekezi huku wakiwa na uhakika wa safari zao.

Wakati huhuo wadau waliotembelea maonesho hayo kwa nyakati tofauti wametoa pongezi kwa LATRA kwa ubunifu na matumizi ya mifumo ya TEHAMA ambayo imewarahisishia upatikanaji wa huduma na taarifa mbalimbali zinazohusu sekta ya usafiri ardhini.

Bw. Paschal Mayalla, Mdau wa usafiri ardhini amesema, Mfumo wa Safari Tiketi umeboresha huduma za usafiri ardhini kwa kumuwezesha abiria kukata tiketi ya safari kwa njia ya mtandao na kupanga safari yake kwa uhakika na kulipa nauli iliyoidhinishwa na LATRA, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo baadhi ya watoa huduma walipandisha nauli kiholela hasa wakati wa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

"Leo hii mwananchi hahitaji tena kuwahi stendi ili kukata tiketi, kupitia mfumo wa Safari Tiketi anaweza kukata tiketi akiwa nyumbani au popote alipo. Hili ni jambo kubwa ambalo limewarahisishia wananchi na linaonesha namna LATRA ilivyoboresha huduma za usafiri ardhini, nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya," amesema Bw. Mayalla.

Kwa upande wake, Bi. Sia Mboya amesema, amevutiwa na Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) https://pis.latra.go.tz/ unaomwezesha mwananchi kufuatilia taarifa muhimu za safari ikiwemo mahali basi lilipo, mwendokasi wake pamoja na muda ambao basi linatarajiwa kufika kituoni.

"Sikuwahi kujua kwamba naweza kufuatilia taarifa za safari kwa kuingiza namba ya usajili wa basi kwenye mfumo huu, ni huduma muhimu inayoongeza usalama na kuwapa wananchi amani wanapokuwa safarini," amesema Bi. Mboya.

Bw. Manyenye Masalu amesema Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) umeongeza imani kwa wananchi kwa kuwa unaiwezesha LATRA kufuatilia mwenendo wa mabasi muda wote yanapokuwa safarini, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa abiria na kuhakikisha madereva wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri.

Pia, Bi. Merygoreth Moshi amesema kupitia Mfumo wa e-Mrejesho pamoja na namba za huduma kwa wateja LATRA 0800110019 / 0800110020 anaweza kuwasilisha maoni, pongezi, mapendekezo na malalamiko kuhusu huduma za usafiri ardhini wakati wowote kimtandao. 

LATRA inaendelea kuwafikia wadau kwa kutoa elimu kuhusu majukumu yake ya kiudhibiti na matumizi ya mifumo ya kidigiti inayorahisisha utoaji wa huduma kupitia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano, ikiwemo kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) viwanja vya Dkt. John S. Malecela, Dodoma, kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026. Kupitia maonesho hayo, wananchi na wadau wanapata fursa ya kujifunza na kujionea kwa vitendo jinsi mifumo ya TEHAMA ya LATRA inavyorahisisha upatikanaji wa huduma za kiudhibiti, kuimarisha uwazi na uwajibikaji, kuongeza usalama wa abiria pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma katika sekta ya usafiri ardhini nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor