Theophilly Mushi, Daktari Bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) amewaasa watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutosubiri dalili za magonjwa ndipo waende hospitali bali wawe na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kutambua mapema viashiria muhimu vya mwili vinavyoweza kusababisha magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Dkt. Mushi amesema hayo Aprili 25 na 26, 2026 alipotoa elimu ya afya kwa watumishi wa LATRA Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Menejimenti ya Mamlaka hiyo kwa watumishi wake kwa lengo la kuongeza uelewa wa wafanyakazi hao kuhusu magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza pamoja na namna ya kujikinga ili kuimarisha afya zao na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Dkt. Mushi amesema ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya ya moyo mapema na kuchukua tahadhari kabla ya ugonjwa kufikia hatua ya hatari kwa kuwa watu wengi hupata matatizo ya moyo bila kutambua dalili au chanzo chake mapema, “unaweza kujikuta unapata maumivu ya kifua kutokana na kubanwa kwa mishipa inayosafirisha damu kwenda kwenye moyo kwa sababu ya mafuta mengi mwilini hali inayoweza kusababisha ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo kuziba,” amesema Dkt. Mushi.
Amefafanua kuwa, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo kunatokana na mafuta mengi mwilini pia ni moja ya sababu kubwa ya maumivu ya kifua na matatizo ya moyo hivyo wasisubiri kupata dalili kama kuvimba miguu, kushindwa kutembea au kupooza upande mmoja wa mwili kwani wakati huo madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi.
Kwa nyakati tofauti, watumishi wa Mamlaka hiyo wameishukuru Menejimenti kupitia CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA kwa kuwezesha watumishi kupatiwa mafunzo hayo ambayo yamewakumbusha kuhusu umuhimu wa kufuatilia afya zao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Bw. Deusdedity Masemba, Afisa Uhusiano LATRA, amebainisha kuwa mafunzo hayo yamempa uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara kama sehemu ya ustawi wa wafanyakazi mahali pa kazi
Naye Bw. Denis Daudi, Afisa Leseni na Usajili LATRA, amesema mafunzo hayo yamewasaidia wafanyazi hao kuelewa namna ya kujikinga na magonjwa yanayoathiri utendaji kazi wa mwili.
“Tumepata elimu ya kujikinga na magonjwa yanayotokana na mtindo mbaya wa maisha na yale yasiyoambukiza yanayoathiri afya na utendaji kazi. Elimu hii itatusaidia kuchukua tahadhari mapema”, amesema Denis.

