Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), mdhibiti wa usafiri wa ardhini Tanzania Bara, ilishiriki katika Mkutano na Maonesho ya Land-Linked Zambia yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Lusaka kuanzia tarehe 23 hadi 24 Aprili 2026. Mamlaka ilitumia fursa hiyo kufanya maonesho, kushiriki katika mijadala, kubadilishana uzoefu, na kujenga mitandao na wadau wa kikanda.
Ikiendana na kaulimbiu isemayo, “Zaidi ya Mipaka: Kufikiria Upya Shoroba za Usafiri za Afrika kwa Ustawi,” Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA, Dkt. Habibu Suluo, aliwasilisha uzoefu wa LATRA na mipango ya kimkakati inayotumia teknolojia kwa wadau mbalimbali, wakiwemo Mhe. Museba Frank Tayali (MB), Waziri wa Uchukuzi na Logistiki wa Zambia, Wakili Flory Okonge, Katibu Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Usafiri wa Ukanda wa Kati (CCTFA) na Bw. Raymond Shoniwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Reli Kusini mwa Afrika (SARA). Masuala muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na changamoto za kuvuka mipaka, udhibiti wa uchovu wa madereva, na urahisishaji wa biashara, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kukuza biashara za mipakani.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa LATRA, Bw. Salum Pazzy, alishirikiana na zaidi ya wadau 300 waliotembelea banda la maonesho la LATRA. Wageni hao walitoka nchi mbalimbali za kikanda, zikiwemo Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Msumbiji, Angola, Namibia, Misri, Zimbabwe na Tanzania. Wengi wao walionesha kuvutiwa na usanifu wa mifumo ya kidijitali ya LATRA, ikiwemo mfumo tumizi wa LATRA, Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS), matumizi ya vitufe vya utambuzi kwa madereva na mfumo wa tiketi za kielektroni (Safari Tiketi).
Kwa ujumla, ushirikiano na wadau wa kikanda kupitia majukwaa ya majadiliano na kubadilishana maarifa umeonesha kuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza mifumo ya shoroba za usafiri barani Afrika na kukuza ustawi wa kikanda. Taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Wizara ya Uchukuzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wakala wa Uwezeshaji Usafiri wa Ukanda wa Kati, Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania, pamoja na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation.

