
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kushirikiana na Chama cha Ushirika cha Madereva na Wamiliki wa Bodaboda na Bajaji Mkoani Kilimanjaro (KIBABOT SACCOS), Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Bararanani Mkoani humo, imetoa elimu ya umuhimu wa kujiunga katika vyama vya ushirika kwa Madereva na Wamiliki wa Pikipiki za Magurudumu Mawili na Matatu Wilayani Mwanga Mkoani kilimanjaro, Juni 06, 2025.
Akizungumza katika Mkutano huo, DCP Johansen Kahatano Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA amesema, Mamlaka imelenga kuwawezesha kiuchumi maafisa wasafirishaji wilayani humo kupitia vyama vya ushirika kwani kupitia vyama hivyo Mamlaka itawarejeshea asilia 20 ya mapato ya leseni za LATRA watakazozikata kupitia ushirika wao hivyo ni muhimu kwa maafisa usafirishaji hao kujiunga na chama cha ushirika.
“Tunataka kutengeneza ajira endelevu kwenu ninyi maafisa wasafirishaji ili mjitegemee kiuchumi, hii ni fursa pana nasi tunapenda iwanufaishe wote na mfahamu tu kuwa Serikali yenu inataka mheshimike kwa kuwa kazi yenu ni sawa na kazi nyingine, pia mtekeleze majukumu yenu kwa kufuata Sheria na Taratibu za usafiri ardhini zilizopo,” ameeleza DCP Kahatano.
Pia, DCP Kahatano amempongeza na kumshukuru Mhe. Joseph Tadayo, Mbunge wa Jimbo la Mwanga ambaye baada ya kuona KIBABOT SACCOS inafanya vizuri Wilayani Moshi, akaona ni fursa ya kipekee kwa maafisa wasafirishaji jimboni kwake kujiunga na SACCOS hiyo ili kubadili maisha yao kiuchumi na kijamii.
Akizungumza na maafisa wasafirishaji, Mhe. Tadayo, Mbunge wa Jimbo la Mwanga amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anataka vijana wawezeshwe ili kujikwamua kiuchumi, hivyo kupitia KIBABAOT SACCOS, jambo hilo linaenda kuwanufaisha vijana Wilayani hapo.
“Serikali ipo tayari kuwawezesha lakini kwa utaratibu, hivyo mimi nitawalipia kiingilio ili wote muweze kujiunga na KIBABOT SACCOSS, hii ni fursa nzuri kwenu ninyi kama vijana na Serikali inawategemea katika ujenzi wa Taifa hili, hivyo kupitia ushirika huu mtakuwa wamoja na kufanya maendeleo kwa pamoja,” amesema Mhe. Tadayo.
Naye Bw. Hamad Bendera, Mwenyekiti wa Bodi ya KIBABOT SACCOS amesema kuwa, LATRA iliwapelekea wazo la kuanzisha ushirika, wakalipokea na kulifanyia kazi na hadi sasa ushirika wao umesajiliwa na umeanza kufanya kazi.
“Tulipopata wazo na kuona lina tija, tulijikusanya watu 68 na kwenda kusoma masuala ya ushirika kwenye Chuo Kikuu cha cha Ushirika Moshi, kwa hiyo tunaendesha ushirika wetu kwa ueledi wa hali yajuu. Pia, tumeweza kuajiri wataalam wengine, kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji na hatimaye tuweze kujisimamia wenyewe ili tufikie malengo tuliyojiwekea ya kuinuana kiuchumi na kijamii,” amesema Bw. Bendera.
Vilevile Bw. Bendera amesema KIBABOT SACCOS imedhamiria kufungua tawi lake la kwanza Wilayani Mwanga na hivyo amewasihi maafisa usafirishaji Wilayani humo kujiunga na ushirika huo ili waweze kuboresha maisha yao kwa kuwa kupitia umoja huo, wataweza kukopesheka kirahisi, watakopeshana na pia kufanya uwekezaji kwenye maeneo tofauti ili kujikwamua kiuchumi.
Nao maafisa wasafirishaji waliohudhuria mkutano huo, wamesema wamepokea kwa dhati fursa hiyo ya kujiunga na KIBABOT SACCOS na wanaimani kubwa kuwa wanaenda kuboresha hali za maisha yao na familia zao kwa kuwa watanufaika moja kwa moja na ushirika kwa kukopa na kufanya uwekezaji.
Kanuni za LATRA za Usafiri wa Magari ya Kukodi, 2020 ilifanyiwa marekebisho Machi, 2023 na kuruhusu LATRA kukasimu madaraka ya kutoa leseni kwa Wakala aliyethibitishwa ambao ni Vyama Ushirika, Taasisi za Umma (LGA), Kampuni na Watu Binafsi.
Chama cha Kwanza cha Ushirika Kilimanjaro (KIBABOT SACCOS LTD) ilisajiliwa 3 Agosti 2023. Kwa sasa Wanatoa Leseni za LATRA kwa Pikipiki kutumia Mfumo wa LATRA wa kutoa leseni (RRIMS) na wamepata fursa ya kuaminiwa na Taasisi zingine za umma na kupewa kazi zinazowaingizia mapato, mfano: kusimamia huduma za uegeshaji magari (parking).