Bw. Abdallah Mitawi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, amewaasa madereva wa mabasi ya masafa marefu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za usalama barabarani, akisisitiza kuwa, mwenendo wao wakati wa safari unafuatiliwa wakati wote kupitia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Bw. Mitawi ameyasema hayo Agosti 26, 2026, alipofanya ziara ya kujifunza majukumu yanayotekelezwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam. Ziara hiyo imehusisha kutembelea Kituo cha Kutahini Madereva, Kituo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) pamoja na Studio ya Uzalishaji Vipindi vya Elimu kwa Umma.
“Nitoe wito kwa madereva kwamba, mienendo yao inaonekana na kujulikana. Kitakachofuata ni kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo, nawasihi kufuata Sheria bila shuruti, wakijua kuwa Serikali ipo macho na inaona mienendo yao wakati wote wa safari,” amesema Bw. Mitawi.
Aidha amesema, matumizi ya teknolojia katika ufuatiliaji wa magari yanapokuwa safarini ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa mfumo wa VTS unaiwezesha LATRA kufuatilia mwenendo wa magari ya abiria, hususan mabasi ya masafa marefu, ikiwemo ufuatiliaji wa mwendokasi na kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa safari.
Katika hatua nyingine, Bw. Mitawi amewataka wamiliki wa mabasi kutimiza wajibu wao wa kuwafuatilia mienendo ya madereva wanaowaajiri, akisisitiza kuwa jukumu la kuhakikisha usalama wa abiria na uzingatiaji wa Sheria si la dereva pekee bali pia linamhusu mmiliki wa chombo na anaweza kuwajibishwa iwapo atashindwa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha dereva anasimamiwa ipasavyo.
“Jukumu la kusimamia usalama wa abiria wawapo safarini si la dereva peke yake, ndio maana wamiliki mmepewa uwezo wa kuyafuatilia magari yenu kupitia simu zenu au kompyuta, Serikali haina nia ya kumfungia dereva au gari, nia ni kuwalinda watu wengi zaidi, lakini pia kulinda rasilimali za nchi ambazo Serikali imewekeza fedha nyingi katika kujenga na kuboresha miundombinu ya sekta ya usafiri ardhini,” amesema Bw. Mitawi.
LATRA inaendelea kushirikiana na watoa huduma za usafiri ardhini kuhakikisha usafiri ardhini unakuwa salama, wenye kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu zilizowekwa na kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya usafiri ardhini.

