Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imebainisha kuwa, urasimishaji wa maafisa usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili (Bodaboda) na utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa maafisa hao ni nguzo muhimu ya kuimarisha udhibiti wa vurugu na ukiukwaji wa Sheria unaofanywa na baadhi ya waendesha pikipiki barabarani.
Hayo yamebainishwa na Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, Februari 19, 2026 katika kipindi cha dakika 45, kituo cha habari ITV ambapo mada ilikuwa nini kifanyike kudhibiti vurugu za waendesha bodaboda barabarani kwa usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.
Bw. Pazzy ameeleza kuwa, Serikali kupitia LATRA imepiga hatua kubwa katika kurasimisha shughuli za bodaboda na kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia SACCOS hali iliyoongeza usalama, nidhamu na ustawi wa waendesha pikipiki pamoja na watumiaji wengine wa barabara.
“LATRA imewarasimisha waendesha bodaboda kwa kuwatambua kupitia vyama vya ushirika kwa mujibu wa Kanuni za Mamlaka, hatua inayowapa hadhi na heshima kama ajira nyingine rasmi. Kupitia urasimishaji huu, waendesha bodaboda wamewezeshwa kuwa mawakala wa utoaji wa leseni za LATRA na wanapata gawio la asilimia 20 kama kamisheni ambayo inawasaidia kujikwamua kiuchumi na kujisimami wao wenyewe,” amesema Bw. Pazzy.
Ameongeza kuwa, kwa sasa LATRA ina mawakala zaidi ya 40 nchi nzima, na kwamba kwa mwezi wa Januari pekee jumla ya shilingi milioni 89 zililipwa kwa mawakala wa vyama vya usafirishaji kama gawio la asilimia 20 ya makusanyo ya leseni za LATRA, hali inayochangia kuheshimika na kuwafanya wajisikie wenye thamani wanapokuwa barabarani.
Vilevile amesema, LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, inaendelea kuweka mifumo ya usajili itakayowawezesha waendesha bodaboda kupata leseni popote walipo, sambamba na kuendelea kuwafikia na kuwapatia elimu ya usalama barabarani nchi nzima kupitia vyama vyao.
Kwa upande wake, SSP Solomon Mwangalimo, Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni, amesema bodaboda ni chombo cha moto kwa umma, hivyo ni lazima waendeshaji wake wazingatie Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa. Dereva wa bodaboda anatakiwa kuwa na leseni halali ya kuendesha chombo, bima, pamoja na kuhakikisha pikipiki ina ubora unaoruhusu kuendeshwa barabarani bila kuhatarisha maisha ya wengine.
Vilevile SSP Mwangalimo amesema, Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kimeanzisha madawati ya elimu ya usalama barabarani kuanzia ngazi ya kata, wilaya hadi taifa, kwa lengo la kuwajengea uwezo waendesha bodaboda kuhusu Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji salama.
“Tangu kuanza kutoa elimu, tumeshuhudia kupungua kwa ajali na vurugu. Zamani bodaboda walikuwa wakisababisha ajali na kuanzisha vurugu, lakini sasa uelewa umeongezeka. Pia Jeshi la Polisi linaendelea kufanya operesheni dhidi ya wavunjaji wa Sheria, na wale wanaokamatwa hupelekwa katika madawati ya elimu ili kuwajenga na kuwabadilisha kitabia,” amesema SSP Mwangalimo.
Naye Bw. Mathias Kasabuku, Katibu wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki (CMPD) Wilaya ya Kigamboni, amesema elimu inayotolewa kupitia vyama vya bodaboda imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vurugu na kuboresha uendeshaji wa huduma hiyo na kuongeza nidhamu na heshima kwa waendesha Bodaboda.
Bw. Kasabuku ameongeza kuwa, licha ya changamoto za gharama za mafunzo na uendeshaji, viongozi wa vyama wanaendelea kuweka mikakati ya kuwafikia madereva kuanzia ngazi za chini hadi za juu ili kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inawafikia madereva wote wanaoendesha Bodaboda.
LATRA inaendelea kufanya juhudi za kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini ili kupunguza athari zitokanazo na uendeshaji hovyo wa vyombo vya moto kibiashara

