Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendelea kuandaa na kutekeleza mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji nchini kwa lengo la kudhibiti ajali za barabarani zinazosababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na upotevu wa nguvu kazi ya Taifa.
Mhe. Kihenzile ametoa agizo hilo Julai 6, 2026, alipotembelea LATRA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, yenye kaulimbiu isemayo "Hii ni Kubwa Kuliko."
Amesema ukuaji wa sekta ya usafiri umeenda sambamba na ongezeko la vyombo vya usafiri pamoja na watumiaji wa huduma hizo, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo na mikakati ya usimamizi wa usalama barabarani ili kupunguza na hatimaye kutokomeza ajali.
"Ni lazima tukubaliane kuwa usafiri wa ardhini umeongezeka, vyombo vya usafiri vimeongezeka na wasafiri wameongezeka. Mmeweka mifumo mingi mizuri, lakini ni muhimu kuendelea kuja na mipango madhubuti ya kuimarisha sekta ya usafirishaji nchini ili kudhibiti ajali za barabarani. Katika ajali hizi wanapoteza maisha watu wasio na hatia na Taifa linapoteza nguvu kazi muhimu. Mnatakiwa kujipanga vizuri kila mwaka na kila wakati ili muwe imara zaidi kuliko jana, lengo letu ni kufikia mahali ambapo ajali za barabarani zitakuwa historia nchini," amesema Mhe. Kihenzile.
Aidha, amesisitiza kuwa jukumu la kudhibiti ajali si la taasisi za Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mtanzania kuhakikisha Sheria na Kanuni za usalama barabarani zinazingatiwa.
Pia amesema ajali nyingi zinaweza kuzuilika kwa kuhakikisha kunakuwa na madereva wenye sifa, ujuzi na wanaozingatia sheria za usalama barabarani.
"Napenda kuwaambia Watanzania kuwa ni wajibu wetu sote kushiriki katika kudhibiti ajali, ajali nyingi zinaweza kuepukika iwapo tutakuwa na madereva wenye sifa na wanaozingatia taratibu za barabarani. Wale wasiokuwa na uelewa wa Sheria za barabarani huwatahatarisha hata madereva wanaofuata Sheria. Tukipata madereva bora, tutaimarisha zaidi sekta ya usafiri na usafirishaji nchini," amesema.
Mhe. Kihenzile ameongeza kuwa katika baadhi ya nchi ajali za barabarani ni matukio nadra, huku akisisitiza kuwa si jambo linalopaswa kuonekana la kawaida nchini.
"Lazima tuendelee kujipanga zaidi ili kuokoa maisha ya Watanzania, kuzuia ulemavu unaotokana na ajali na kulinda nguvu kazi ya Taifa inayochangia maendeleo ya nchi," amesema Mhe. Kihenzile.
LATRA kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya usafiri ardhini wanaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kiudhibiti na matumizi ya mifumo ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na matumizi sahihi wa Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i- Button) ili kuhakikisha usalama katika sekta ya usafiri ardhini.

