Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuimarisha usimamizi wa huduma za usafiri wa reli ya kisasa (SGR), pamoja na kutatua changamoto zinazohusiana na mfumo wa ukataji wa tiketi za SGR ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora, salama na zenye kuaminika.
Mhe. Kihenzile ametoa maelekezo hayo Julai 6, 2026 kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam alipoitembelea LATRA ambapo alieleza kuwa, kumekuwa na malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara kutoka kwa watumiaji wa huduma za SGR ikiwemo abiria kukosa nafasi za kusafiri na treni licha ya kuwa treni inaondoka bila abiria huku mfumo ukionesha treni imejaa.
Vilevile amesema, LATRA inapaswa kufuatilia kwa karibu changamoto zote zinazojitokeza katika huduma za reli na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
"Mnalazimika kufuatilia kwa ukaribu changamoto zinazojitokeza katika huduma za SGR na kumjulisha Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi hatua mnazozichukua kila mara. Pia muwaweke wazi wananchi kuhusu hatua hizo ili wajue Serikali inaendelea kuzitatua changamoto zilizopo," amesema Mhe. Kihenzile.
Ameeleza kuwa, huduma za reli ya SGR zimepokelewa vizuri na watanzania kutokana na ubora na mchango wake katika kurahisisha usafiri, hivyo ni muhimu kuhakikisha matarajio ya wananchi yanaendelea kutimizwa kupitia usimamizi madhubuti wa huduma hizo.
Ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika mradi wa reli ya kisasa unapaswa kuendana na utoaji wa huduma bora zinazokidhi viwango vya ubora na ufanisi.
"Watanzania wanaupenda usafiri wa SGR. Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huu, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha huduma zake zinaendelea kutolewa kwa ufanisi na changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa haraka," amesema Mhe. Kihenzile.
LATRA inaendelea kutekeleza jukumu la kudhibiti sekta ya reli nchini kwa kushirikiana na wadau wakiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutatua changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu hatua zinazochukuliwa ili kuendelea kujenga imani kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa reli nchini.

