Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. KIHENZILE: ELIMU YA UTHIBITISHAJI WA MADEREVA NI MUHIMU KWA USALAMA WA WATANZANIA
Imewekwa: 09 Jul, 2026
MHE. KIHENZILE: ELIMU YA UTHIBITISHAJI WA MADEREVA NI MUHIMU KWA USALAMA WA WATANZANIA

Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu dhamira ya Serikali ya kuthibitisha madereva wa vyombo vya moto vya kibiashara, hatua inayolenga kuimarisha taaluma ya udereva na kuongeza usalama wa wananchi.

Mhe. Kihenzile ametoa maelekezo hayo Julai 6, 2026 alipoitembelea LATRA kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere ambapo aliielekeza LATRA kuendelea kushughulikia na kujibu malalamiko yanayowasilishwa na wananchi kwa majibu yanayojitosheleza ili kuondoa sintofahamu kuhusu suala la uthibitishaji wa madereva.

Mhe. Kihenzile amesema, LATRA inapaswa kuwaeleza wananchi kuwa uthibitishaji wa madereva ni hatua ya kitaalamu inayolenga kuhakikisha madereva wanakuwa na ujuzi na uwezo unaokidhi viwango vinavyohitajika, sawa na taaluma nyingine ambazo zinahitaji uthibitisho wa umahiri wa wataalamu wake.

"Waambieni watu ukweli kuhusu dhamira ya Serikali. Udereva ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine, hivyo lengo la uthibitishaji ni kuhakikisha madereva wanakuwa na uwezo unaohitajika wa kutoa huduma bora na salama kwa wananchi," amesema Mhe. Kihenzile.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwaeleza madereva utaratibu uliowekwa ili kuwaondolea hofu. Amesema maswali ya mtihani wa uthibitishaji yameandaliwa kwa kuzingatia maarifa na stadi za vitendo katika udereva, ikiwemo uelewa wa alama na michoro ya barabarani pamoja na Kanuni za usalama barabarani.

"Serikali imeweka utaratibu unaompa dereva fursa ya kufanya mtihani zaidi ya mara moja endapo hatofaulu. Akifeli mara ya kwanza ataruhusiwa kufanya tena mtihani, akifeli mara ya pili atapewa nafasi ya tatu, na asipofaulu anapewa fursa ya kurudi kupata mafunzo ya kurejea (refresher course) kabla ya kufanya mtihani tena ili aweze kufaulu," amesema Mhe. Kihenzile.

LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imeandaa video za elimu zinazowakumbusha madereva kuhusu masuala ya msingi ya kuzingatia wakiwa barabarani ikiwemo suala la alama na michoro na video hizo zinapatikana LATRA Online TV kwenye mtandao wa YouTube zinazowawezesha madereva kujielimisha zaidi katika taaluma yao.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor