Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. MUTASINGWA: ELIMU YA MIFUMO YA LATRA NI MUHIMU KWA WANANCHI
Imewekwa: 17 Feb, 2026
MHE. MUTASINGWA: ELIMU YA MIFUMO YA LATRA NI MUHIMU KWA WANANCHI

Mhe. Mha. Johnston Mutasingwa (Mb) Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (PIC) ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendelea kutoa elimu kuhusu mifumo ya Teknojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotumiwa na Mamlaka katika shughuli zake za kiudhibiti ili kuongeza uwazi, ufanisi na ushiriki wa wananchi katika sekta ya usafiri ardhini.

Mhe. Mutasingwa amebainisha hayo Februari 16, 2026 wakati wajumbe wa Kamati ya PIC walipotembelea ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya ziara maalum ya kujifunza jinsi LATRA inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

“Tunawapongeza LATRA kwa juhudi kubwa za kurahisisha upatikanaji wa taarifa za usafiri ardhini kwa wananchi. Hata hivyo, tunasisitiza muendelee kutoa elimu kwa kuhusu mifumo mnayoitumia ili wananchi waweze kufahamu LATRA inafanya nini na elimu hii ikiwafikia wananchi ambao ndio watumiaji wa huduma za usafiri ardhini maswali mengi ambayo wamekuwa wakijiuliza yatapungua na itaongeza ufanisi katika utendaji kazi wenu,” amesema Mhe. Mtasigwa.

Kwa upande wake, CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amesema kuwa Mamlaka ina mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayorahisishia utoaji wa huduma za usafiri ardhini ikiwemo Mfumo wa Safari Tiketi, unaorahisisha upatikanaji wa tiketi za mabasi ya masafa marefu na usafiri wa Treni ya Kisasa (SGR), Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS), unaomuwezesha abiria kufuatilia mwenendo wa safari na kutambua mahali basi lilipo na Mfumo Tumizi wa LATRA APP, unaomuwezesha abiria kuhakiki tiketi za safari, kupata taarifa za viwango vya nauli za mabasi ya mijini (daladala) na mabasi ya masafa marefu, na wasafirishaji wanaweza kuhakiki uhai wa leseni zao.

Aidha, CPA, Dkt. Suluo ameeleza kuwa LATRA pia inatumia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) ambao ni mfumo mama wa Mamlaka unaosaidia katika usimamizi na udhibiti wa shughuli za usafiri ardhini kwa jumla.

Naye Prof. Ahmed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa LATRA, ameishukuru Kamati ya PIC kwa ziara hiyo na ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa, ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na LATRA katika shughuli zake za udhibiti.

Elimu ya mifumo ya LATRA ni nyenzo muhimu katika kuimarisha udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini na kufanikisha lengo la Serikali la kuwa na huduma za usafiri zilizo salama, bora na endelevu.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo