Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeeleza kuwa, huduma za usafiri wa umma siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 zitaendelea kutolewa kama kawaida.
Hayo yamebainishwa na Bw. Geoffrey Silanda, Meneja Uratibu Usalama na Mazingira LATRA alipozungumza na wanahabari, ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Oktoba 24, 2025 kuhusu utoaji wa huduma za usafiri wa abiria siku ya Uchaguzi Mkuu.
Bw. Silanda amesema kuwa, wapo baadhi ya wapiga kura watakaohitaji kutumia usafiri wa umma ili kufika kwenye vituo vya kupigia kura, hivyo ni wajibu wa Mamlaka kuwezesha jambo hilo pasi na changamoto yoyote.
“Hadi sasa hakuna msafirishaji yeyote aliyewasilisha maombi rasmi ya kusitisha huduma siku ya uchaguzi hivyo tunawasihi wasafirishaji kuendelea kutoa huduma na wananchi waendele kutumia huduma za usafiri wa umma na watumie haki yao ya msingi kikatiba ya kupiga kura,” amesema Bw. Silanda
Kwa upande wake, Bw. Issa Nkya, muweka hazina wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) amesema wamejipanga kutoa huduma za usafiri na usafirishaji na wananchi waondoe shaka kuhusu usafiri kwa kuwa unapatikana saa 24.
“Sisi kama wasafirishaji tumezungumza na tumekubaliana kuendelea kutoa huduma siku ya uchaguzi ingawa baadhi ya makampuni watapunguza idadi ya magari kutokana na idadi ya abiria watakaokuwepo,” ameeleza Bw. Lema
Mamlaka ina wajibu wa kufuatilia huduma za usafiri ardhini na kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ukamilifu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Usafiri Ardhini nchini.

