Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewajengea uwezo wanahabari mabalozi wa LATRA kuhusu Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotumiwa na Mamlaka hiyo katika utekekezaji wa majukumu yake.
Akizungumza kwenye semina ya mafunzo kwa wanahabari mabalozi wa LATRA, iliyofanyika Aprili 1 na 2, 2026 Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha Mkoa wa Pwani CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa, Mifumo ya LATRA imerahisisha utoaji huduma za usafiri kwa wadau wa sekta ya usafiri ardhini kwa kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
“Matumizi ya mifumo ya TEHAMA yameleta mageuzi makubwa katika namna tunavyosimamia sekta ya usafiri ardhini. Leo hii tuna uwezo wa kufuatilia mwenendo wa vyombo vya usafiri kwa karibu zaidi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa viwango vinavyotakiwa, pia imeongeza uwazi na imani kwa wananchi wanaotumia huduma za usafiri ardhini,” amesema Dkt. Suluo.
Amefafanua kuwa, mifumo hiyo inajumuisha Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaomuwezesha abiria kufahamu mahala basi lilipo, Mfumo Tumizi wa LATRA App, Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) ambao ndio Mfumo mama wa Mamlaka na Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaojulikana kwa jina la Safari Tiketi unaomuwezesha abiria kukata tiketi za mabasi na treni.
Vilevile Dkt. Suluo amesema kuwa, matumizi ya teknolojia yameiwezesha LATRA kufuatilia kwa karibu utendaji wa watoa huduma na kuchukua hatua stahiki pale panapobainika ukiukwaji wa Taratibu na Sheria za usafirishaji.
Aidha, amewahimiza wanahabari hao kutumia maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo ili kuelimisha umma kuhusu majukumu ya LATRA na umuhimu wa mifumo hiyo katika kuhakikisha usalama, ubora na unafuu wa huduma za usafiri ardhini. Amesema kuwa ushirikiano kati ya LATRA na vyombo vya habari ni muhimu katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi na kujenga uelewa mpana wa Kanuni na Taratibu zinazosimamia sekta ya usafiri.
Bw. Kulwa Karedia, Mwandishi wa Gazeti la Jamhuri ni miongoni mwa wanahabari mabalozi wa LATRA walioshiriki mafunzo hayo ameipongeza LATRA kwa kuandaa semina hiyo yenye lengo la kuwajengea uwezo ambao utawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa uweledi zaidi.
“Mafunzo haya yametuwezesha kuelewa kwa kina mifumo inayotumiwa na LATRA, jambo litakalotusaidia kuhabarisha umma kwa usahihi zaidi na kuondoa upotoshaji wa taarifa. Pia tutaendelea kushirikiana na LATRA kwa ukaribu zaidi kuelimisha na kuihabarisha jamii kuhusu masuala mbalimblai yanayohusu sekta ya usafiri ardhini,” amesema Bw. Karedia.
Semina hiyo ni sehemu ya jitihada za LATRA za kuimarisha ushirikiano na wadau wake pamoja na kuhakikisha kuwa taarifa kuhusu huduma na mifumo inayotumiwa na Mamlaka zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati.

