Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

JUMUIYA YA SARA YAKOSHWA NA UBORESHAJI WA USAFIRI WA RELI TANZANIA
Imewekwa: 25 Nov, 2025
JUMUIYA YA SARA YAKOSHWA NA UBORESHAJI WA USAFIRI WA RELI TANZANIA

Bw. Raymond Shoniwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Reli Kusini mwa Afrika (SARA) amesema wamekoshwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha sekta ya usafiri wa reli jambo ambalo limerahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Bw. Shoniwa mebainisha hayo Novemba 24, 2025 wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Maadhmisho ya kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini yanayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam ambapo wadau wa usafirishaji wa ndani na nje ya nchi wanatoa elimu na huduma kwa wananchi wanaotembelea viwanjani hapo.

“Nawapongeza sana kwa hatua hii mliyofikia na tunatambua kazi nzuri mnayoifanya kwenye uwekezaji hasa wa sekta ya usafirishaji hasa kwenye usafiri wa reli na kwa haya mnayoyafanya mwakani tutafanya vikao vyetu vya Bodi hapa Tanzania ili na sisi tujifunze zaidi,” ameeleza Bw. Shoniwa.

Kwa upande wake. Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb) Naibu Waziri wa Uchukuzi amesema moja ya maeneo ambayo Serikali imeboresha kwenye upande wa usafiri wa reli ni mabadiliko ya Sheria ya Reli ambayo kwa sasa inaruhusu wawekezaji wa sekta binafsi ndani na nje ya nchi kutoa huduma za usafiri wa reli kwa kutumia miundombinu ya Serikali iliyopo.

“Serikali imeruhusu jambo hili ili kutoa fursa kwa kampuni binafsi kuwekeza kwenye usafirishaji kwa sababu miundombinu inayowezesha huduma hii ipo na tunaamini jambo hili litainua uchumi wa wananchi na Taifa kwa jumla,” amesema Mhe. Kihenzile.

Tanzania inaadhimisha kwa mara ya kwanza Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini  kuanzia Novemba 24 hadi 29 Dar es Salaam ambapo inahusisha maonesho katika viwanja vya Mnazi Mmoja na makongamano yatakayofanyika Novemba 25 hadi 27, 2025 ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam. Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 ni Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo