Mawakala wanaotoa huduma za leseni za usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu (Bodaboda na Bajaji) kwa niaba ya LATRA, wameaswa kuzingatia Sheria, Kanuni na masharti ya uwakala ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, zenye uwazi na zinazozingatia maadili ya kazi.
Akizungumza wakati wa kikao cha mafunzo kwa mawakala hao, Bw. Denis Daudi, Afisa Leseni na Usajili LATRA Mei 21, 2026 ofisi za LATRA Dar es Salaam, amesema kuwa, Mamlaka imewaelekeza mawakala kusimamia misingi ya kisheria iliyopo kwenye leseni zao za uwakala katika utoaji wa huduma za leseni za bodaboda na bajaji.
Bw. Daudi amesema mawakala wana nafasi muhimu ya kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi na kuhakikisha wanawapatia huduma stahiki ikiwemo namba ya malipo kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
“Ni muhimu kwa mawakala kuelewa na kusimamia misingi iliyopo kwenye vyeti vyao vya uwakala ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uweledi, uadilifu, kuzingatia maadili ya kazi pamoja na Sheria na Taratibu za uwakala,” amesema Bw. Daudi.
Vilevile Bw. Daudi amewakumbusha mawakala kushirikiana kwa pamoja wanapotekeleza majukumu yao ili kufikia malengo waliyojiwekea. “Hakikisheni mnashirikiana kutekeleza majukumu yenu kwa pamoja mkizingatia uweledi na misingi ya kazi, na mshirikiane kutatua changamoto zinazowakabili kwa pamoja kwani ndio msingi imara wa kufikia yale malengo mliyojiwekea na kufikia malengo ya Serikali kwa jumla”, amesema Bw. Daudi.
Kwa nyakati tofauti, mawakala hao wameeleza namna mafunzo hayo yalivyowasaidia kuongeza uelewa kuhusu Kanuni na masharti ya utoaji leseni kwa niaba ya LATRA pamoja na wajibu wao wa kutoa elimu kwa wadau wanaowahudumia.
Bw. Abdallah Maulid, wakala wa kutoa leseni za LATRA, ameishukuru Mamlaka kwa kuendelea kuwajengea uwezo kupitia mafunzo mbalimbali yanayowakumbusha umuhimu wa kutoa huduma kwa kuzingatia uweledi, uwazi, taaluma na misingi ya utoaji leseni.
Naye Bw. Jonas Msunga, amesema mafunzo hayo yamewakumbusha namna bora ya kutekeleza majukumu yao ili kuwafikia wananchi kwa wakati na kuhakikisha wasafirishaji wanapata leseni zinazowaruhusu kutoa huduma za usafiri wa abiria kisheria.
LATRA imeendelea kusisitiza umuhimu wa mawakala kuzingatia Sheria, Kanuni na maadili ya kazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuongeza ufanisi, uwazi na kuimarisha imani kwa Mamlaka.

