Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAWAKALA WA LATRA WAONYWA DHIDI YA VITENDO VYA RUSHWA
Imewekwa: 03 Jun, 2026
MAWAKALA WA LATRA WAONYWA DHIDI YA VITENDO VYA RUSHWA

Mawakala wanaotoa huduma za leseni za usafirishaji kwa niaba ya LATRA kwa usafiri wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu (Bodaboda na Bajaji) wameonywa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuzingatia maadili ya kazi wanapotekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.

Hayo yamebainishwa na Bw. Patel Ngereza, Kaimu Meneja Leseni Usafiri wa Barabara LATRA, wakati akitoa mafunzo kwa mawakala hao Mei 21, 2026 ofisi za LATRA Dar es Salaam.

Bw. Ngereza amesema, mawakala wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uweledi na kwa kuzingatia maadili ya kazi kwa kuwa wanaiwakilisha LATRA mbele ya wananchi wanaohitaji huduma za leseni za usafirishaji zilizokuwa bora.

“Mamlaka imepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya mawakala, hali inayochangia kuchafua taswira ya Taasisi. Vitendo hivi havitafumbiwa macho na Mamlaka kwani vinakwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi”, amesema Bw. Ngereza.

Aidha, Bw. Ngereza amesema Mamlaka inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuwakumbusha mawakala hao kuzingatia Sheria, Kanuni na masharti ya cheti cha uwakala walichopewa na LATRA, utoaji wa elimu na maonyo mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye uwazi.

Naye Bw. Augustus Fungo, Afisa Huduma kwa Wateja Mkuu LATRA, amewakumbusha mawakala hao kuwa, huduma za LATRA zinapaswa kutolewa kwa kufuata mifumo rasmi ya malipo na kwamba kupokea fedha taslimu wakati wa utoaji wa huduma ni kinyume na miongozo iliyowekwa na Mamlaka.

Pia amesema, Mamlaka inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kufuatilia utendaji kazi wa mawakala hao ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti waliyopewa wakati wote wanapotoa leseni za usafirishaji kwa niaba ya LATRA.

Kwa upande wake, Bw. Hassan Ramadhan ambaye ni wakala wa kutoa leseni kwa niaba ya LATRA, amesema changamoto ya rushwa imeendelea kuathiri baadhi ya kampuni za uwakala na amewasihi mawakala wenzake kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo ili kulinda heshima ya Mamlaka na Serikali kwa jumla.

Naye Bw. Paul Kigosi, wakala wa kutoa leseni za LATRA, amesema mafunzo waliyopewa yamesaidia kuongeza uelewa kuhusu wajibu wao wa kutoa huduma kwa kuzingatia Sheria, uwazi na uwajibikaji pamoja na namna bora ya kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma za leseni.

LATRA imeendelea kutekeleza juhudi mbalimbali za kuwakumbusha mawakala kutekeleza majukumu yao kwa uwazi bila kujificha na kutotumia udanganyifu wowote kwenye utoaji leseni za usafirishaji kwa niaba ya LATRA.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor