Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAWAJENGEA UWEZO MADEREVA WAKE
Imewekwa: 17 Jun, 2026
LATRA YAWAJENGEA UWEZO MADEREVA WAKE

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inaendesha mafunzo ya wiki mbili kwa madereva wake, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za usalama barabarani, kuwapa ujuzi wa udereva wa kujihami, kuimarisha nidhamu, kuwajengea uelewa wa masuala ya kiitifaki wanapotoa huduma kwa viongozi na watu wenye nyadhifa mbalimbali serikalini na ndani ya Mamlaka.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bw. Athumani Kwikima, Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka LATRA amebainisha kuwa usimamizi madhubuti wa usafiri ardhini unapaswa kuanzia ndani ya taasisi ambapo madereva wake wanatakiwa kuwa na uweledi ili kuongeza ufanisi na kupunguza ajali zitokanazo na makosa ya kibinadamu.

"Mamlaka imeandaa mafunzo haya kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kupunguza kabisa ajali zitokanazo na makosa ya kibinadamu. Matarajio yetu ni kuona mabadiliko makubwa ya kiutendaji na ongezeko la tija mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo haya," ameeleza Bw. Kwikima.

Naye Dkt. Omar Mash, Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi, aliyemwakilisha Mkuu wa Chuo (Taaluma) NIT amepongeza uamuzi wa LATRA wa kuwekeza kwenye rasilimali watu wake na ameeleza kuwa NIT imejipanga vizuri kutoa mbinu za kisasa zitakazowawezesha madereva hao kukabiliana na changamoto za barabarani huku wakihakikisha kuongeza usalama wa vyombo vya moto vya  Serikali, abiria, na watumiaji wengine wa barabara.

“Ni jambo la busara kuhakikisha madereva wanapata mafunzo ya kila mara, hii inasaidia wawe na utimamu wa mwili na akili hivyo kuweza kukabiliana na hali ya dharura pale inapojitokeza, sisi kama NIT tunakwenda kuwafundisha udereva wa kujihami, namna bora na ya kisasa ya kutunza vyombo wanavyovitumia na kujielekeza katika mienedo bora ili kupunguza  ajali zinazoepukika na kuhakikisha usalama wa vyombo na watumiaji wengine,” amesema Dkt. Mash.

Uamuzi huo wa uongozi umepokelewa kwa mwamko mkubwa na madereva wa Mamlaka ambao ndiyo wanufaika wa mafunzo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Bw. Andrea Kasagula, dereva wa LATRA Mkoa wa Shinyanga, ameshukuru kwa fursa hiyo ya kipekee akibainisha kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuwaongezea utulivu wa kiakili wanapotekeleza majukumu yao, kuongeza uweledi wao wa kiutendaji na kuwapa mbinu mpya za kiusalama ambazo hawakuwa nazo hapo awali.

Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia Juni 15 hadi 28, 2026 ukumbi wa mikutano Ofisi ya LATRA Mkoa wa Morogoro yakijumuisha nadharia na vitendo chini ya usimamizi wa wakufunzi wabobezi wa masuala ya usafirishaji nchini kutoka NIT.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor