Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAWAJENGEA UWEZO POLISI KUSIMAMIA VTS
Imewekwa: 03 Mar, 2026
LATRA YAWAJENGEA UWEZO POLISI KUSIMAMIA VTS

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kuwajengea uwezo maafisa wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) hatua inayolenga kuongeza usalama wa vyombo vya moto vinavyodhibitiwa nchini.

Hayo yamebainishwa na Bw. Mbwana Ndaro, Afisa Mfawidhi Kituo cha VTS wakati wa ziara ya mafunzo ya Maafisa hao kutoka mikoa ya Lindi na Njombe walipotembelea Kituo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) cha LATRA kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam Februari 24, 2026.

Bw. Ndaro, amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha udhibiti wa usalama barabarani kupitia matumizi ya teknolojia, hususan katika kudhibiti mienendo isiyofaa ya madereva wa vyombo vya moto vinavyodhibitiwa na LATRA. Ameongeza kuwa, Mamlaka inaendelea kushirikiana kwa karibu na maafisa hao ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya usafiri ardhini.

“Mafunzo haya tuliyoyatoa kwa maafisa wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani yamewajengea uwezo mkubwa ambao utawezesha kufuatilia kwa ufanisi magari na mienendo ya madereva wanaodhibitiwa wanapotekeleza majukumu yao ya kuhakikisha usalama barabarani,” amesema Bw. Ndaro.

Ameongeza kuwa, mfumo huo unawezesha LATRA kuchukua hatua stahiki pale panapobainika ukiukwaji wa Sheria au Kanuni za usalama barabarani, jambo linalochangia kuimarisha nidhamu kwa madereva na kulinda maisha ya abiria pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Kwa upande wake, SP James Makumu, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Lindi, ameishukuru LATRA kwa kutoa mafunzo hayo akisema yataongeza ufanisi katika usimamizi wa usalama barabarani, huku akiwataka wasafirishaji kuzingatia Sheria na kuhakikisha usalama wakati wa safari.

“Tunaishukuru LATRA kwa mafunzo haya, tumekuwa tukishirikiana katika nyanja mbalimbali za kazi zetu, na kupitia mafunzo haya tumeweza kupata uelewa na ujuzi zaidi kuhusu namna ya kusimamia Mfumo wa VTS. Hii itaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu. Nitumie fursa hii kuwasihi wasafirishaji wote kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani ili kulinda usalama wa abiria na mali zake,” amesema SP Makumu.

Ziara hiyo imelenga kuwapatia maafisa hao mafunzo ya kina kuhusu namna Mfumo wa VTS unavyofanya kazi kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo, ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na udhibiti wa usalama barabarani nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo