Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAPEWA KONGOLE USHIRIKIANO NA WANAHABARI
Imewekwa: 22 Apr, 2026
LATRA YAPEWA KONGOLE USHIRIKIANO NA WANAHABARI

Wanahabari mabalozi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) wameipongeza LATRA kwa kuendelea kushirikiana nao kupitia mafunzo yanayowawezesha kufikisha habari kwa kuzingatia uweledi, ukweli, usahihi huku wakihimiza umoja, mshikamano na uzalendo kwa watanzania.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa semina ya mafunzo kwa wanahabari mabalozi wa LATRA iliyofanyika Aprili 1 na 2, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani ambapo walipata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya usafiri ardhini nchini.

Bw. Superius Ernest, Mwanahabari balozi wa LATRA amesema kuwa, Mamlaka imekuwa ikiwapa ushirikiano wa karibu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao ya kuhabarisha na kuelimisha jamii

“LATRA wamekuwa wakitupa ushirikiano sana mathalan ikitokea tunahitaji ufafanuzi wa jambo fulani huwa tayari kujibu hata kwa njia ya simu. Wakati mwingine hata viongozi wanapokuwa kwenye vikao, wakipata nafasi hupokea simu na kutoa majibu ya kina. Hili limetusaidia kutekeleza wajibu wetu kwa ufanisi”, amesema Bw. Ernest.

Naye Bi. Esterbella Malisa, Mwanahabari balozi wa LATRA amefafanua namna LATRA inavyotoa ushirikiano kwa wanahabari wakati wowote na mahala popote.

“LATRA inastahili pongezi, wamekuwa karibu sana na sisi wanahabari kila tunapohitaji taarifa kutoka kwao tunazipata kwa wakati, wana majibu ya swali lolote utakalowauliza ushirikiano wao ni mkubwa sana na hakuna siku wametuangusha”, amesema Bi. Malisa.

Aidha Bi. Malisa amebainisha kuwa, mafunzo waliyoyapata yataboresha uandishi wao kwa kuwa wamejengewa uwezo uelewa mpana wa masuala ya usafiri ardhini na hivyo yatasaidia kutoa taarifa sahihi za masuala ya sekta ya usafiri na usafirishaji kwa wadau wa Mamlaka hiyo.

Wakati huohuo Bi. Zaujia Swaleh, Mwanahabari balozi wa LATRA amesema maarifa waliyoyapata kuhusu Sheria, Kanuni na Taratibu za usafirishaji zitawawezesha kutoa habari kwa kina na kwa usahihi.

LATRA imeendelea kushikiana na vyombo vya habari nchini kuwawezesha kupata taarifa sahihi kwa wakati hatua inayochangia kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha usalama katika sekta ya usafiri ardhini nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo