Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAENDELEA KUIMARISHA UDHIBITI WA USAFIRI ARDHINI KUPITIA TEHAMA
Imewekwa: 13 Aug, 2026
LATRA YAENDELEA KUIMARISHA UDHIBITI WA USAFIRI ARDHINI KUPITIA TEHAMA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kuimarisha udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini nchini kupitia matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usimamizi, kuimarisha usalama na kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya usafiri ardhini nchini.

Hayo yamebainishwa na CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA hivi karibuni wakati alipotembelea banda la LATRA lililopo viwanja vya John Malecela jiji Dodoma Kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026.

Dkt. Suluo amesema matumizi ya TEHAMA yameiwezesha LATRA kupata na kutumia taarifa kwa wakati, kufuatilia utendaji wa watoa huduma na vyombo vya usafiri vinavyodhibitiwa na LATRA, na kuchukua hatua stahiki pale inapobainika ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia sekta ya usafiri ardhini.

Amebainisha mifumo hiyo kuwa ni Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS), Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS), LATRA App na Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaojulikana kama Safari Tiketi.

“Matumizi ya TEHAMA yamekuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa majukumu ya LATRA, ambapo Mamlaka imeendelea kutumia mifumo mbalimbali ya kidigiti katika kusimamia huduma za usafiri wa barabara na reli. Mifumo hiyo imewezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, ufuatiliaji wa vyombo vya usafiri na kurahisisha huduma kwa wasafirishaji pamoja na watumiaji wa usafiri”, amesma Dkt. Suluo.

Vilevile amesema, VTS inaiwezesha LATRA kufuatilia mwenendo wa magari yanayofanya shughuli za usafirishaji, jambo linalosaidia usimamizi wa usalama barabarani na uzingatiaji wa taratibu za usafirishaji wakati Mfumo wa PIS unamwezesha abiria kupata taarifa muhimu kwa wakati kuhusu safari, ikiwemo eneo ambalo basi lilipo, muda wa kufika katika kituo husika na mwendokasi wa basi.

Pia, ameeleza Mfumo wa RRIMS ni mfumo mama wa LATRA ambao umeongeza kasi ya utoaji wa huduma na kupunguza utegemezi wa michakato ya kawaida inayoweza kuchukua muda mrefu. Na kupitia mfumo huu kati ya mwezi Julai 2025 na Machi 2026, LATRA ilifanikiwa kutoa jumla ya leseni 388,715, ikiwa ni ongezeko la asilimia 55 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Adha, Dkt. Suluo amesema, Mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu matumizi ya mifumo hiyo ili kuhakikisha teknolojia iliyowekezwa inatumika kikamilifu na wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na huduma zinazotolewa kimtandao.

Ameongeza kuwa, Mamlaka inaendelea kuboresha mifumo hiyo na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazopatikana kimtandao ikiwa ni sehemu ya ya juhudi za Serikali za kujenga huduma za usafiri ardhini zilizo salama, bora, za uhakika na zinazozingatia mahitaji ya wananchi.

LATRA inaendelea kutumia TEHAMA kuimarisha udhibiti, kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma, pamoja na kujenga sekta ya usafiri ardhini inayotumia taarifa, teknolojia na ubunifu katika kukidhi mahitaji ya wananchi na wadau.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor