Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya usafiri ardhini, wakiwemo watoa huduma na watumia huduma za usafiri ardhini, kuhusu majukumu yanayotekelezwa na LATRA pamoja na maboresho yanayotekelezwa na Serikali ili kuongeza uelewa na ushiriki wao katika kuendeleza sekta ya usafirishaji nchini.
Mhe. Kihenzile ametoa maelekezo hayo alipoitembelea LATRA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Juni 6, 2026 yaliyofanyika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, ambapo alipata fursa ya kushuhudia huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka pamoja na mifumo ya kidigiti inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa LATRA kukutana ana kwa ana na wadau mbalimbali, kusikiliza maoni yao na kutoa elimu kuhusu majukumu ya Mamlaka pamoja na jitihada za Serikali za kuendelea kuboresha huduma za usafiri ardhini.
"Endeleeni kutoa elimu kwa wadau wanaoitembelea LATRA ili wafahamu majukumu ya kiudhibiti mnayotekeleza. Pia waelezeni maboresho mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali, hususan huduma za usafiri wa saa 24 ambazo zimeongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma za usafiri na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi," amesema Mhe. Kihenzile.
Aidha, amesema utoaji wa elimu kwa wadau ni nyenzo muhimu katika kuongeza uwelewa mpana kuhusu matumizi sahihi ya huduma zinazodhibitiwa na LATRA, kuimarisha usalama wa usafiri na kuendeleza ushirikiano kati ya Mamlaka na wadau hao.
Kwa upande wake, Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, amesema kuwa, Mamlaka inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yanayotekelezwa, huduma zinazotolewa, mifumo ya kidigiti inayorahisisha utoaji wa huduma pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha usalama, ufanisi na upatikanaji wa huduma za usafiri ardhini.
Ameongeza kuwa, pamoja na maonesho hayo, LATRA inaendelea kuwafikia wananchi kupitia tovuti ya Mamlaka, mitandao ya kijamii na vipindi vya runinga vinavyorushwa kupitia TBC1 na Clouds TV kila Jumanne, ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka na mchango wa Mamlka katika maendeleo ya sekta ya usafiri na usafirishaji nchini.
LATRA inashiriki kila mwaka katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu huduma zake, kupokea maoni ya wadau na kuonesha mifumo mbalimbali ya kidigiti inayorahisisha utoaji wa huduma na kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri ardhini.

