Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MKURUGENZI MKUU LATRA AWAKUMBUSHA WATUMISHI KUZINGATIA MISINGI YA HUDUMA BORA KWA MTEJA
Imewekwa: 26 Aug, 2026
MKURUGENZI MKUU LATRA AWAKUMBUSHA WATUMISHI KUZINGATIA MISINGI YA HUDUMA BORA KWA MTEJA

CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amewakumbusha watumishi wa Mamlaka kuendelea kuzingatia misingi ya Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (Quality Management System – QMS) katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa kumjali mteja na kumpatia huduma bora ni msingi muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa LATRA na Serikali kwa ujumla.

CPA, Dkt. Suluo amesema utoaji wa huduma unaozingatia QMS unamtaka kila mtumishi kumweka mteja katika kiini cha huduma, kuonesha uongozi katika nafasi yake, kushirikiana na wengine, kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi, kujenga na kusimamia mahusiano mazuri na wadau pamoja na kuendelea kutafuta fursa za kuboresha huduma.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao kazi cha watumishi wa LATRA kutoka Idara ya Barabara, kilichofanyika Agosti 20 na 21, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la NSSF, Morogoro.

Akizungumzia msingi wa kumjali mteja, CPA, Dkt. Suluo amewataka watumishi kuhakikisha huduma wanazotoa si tu zinakidhi mahitaji ya wananchi, bali zinajenga uzoefu mzuri na, inapowezekana, kuvuka matarajio yao.

“Tunapomhudumia mwananchi, tunapaswa kuhakikisha tunatoa huduma bora inayovuka matarajio yake, kwa sababu kila mtumishi wa LATRA ni sehemu muhimu ya taswira ya Mamlaka na Serikali kwa ujumla. Haina haja ya kuwa mkali; badala yake, tumia fursa hiyo kutoa elimu zaidi na kutafuta suluhu,” amesema CPA, Dkt. Suluo.

Amesisitiza kuwa mtumishi anapokutana na mwananchi mwenye changamoto hapaswi kuishia katika kueleza kanuni au kumuonesha asichoweza kufanya, bali anapaswa kumsikiliza, kumwelewa, kumpatia elimu na kumsaidia kupata suluhu ndani ya Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Kuhusu msingi wa uongozi (Leadership), CPA Dkt. Suluo amewakumbusha watumishi kuwa uongozi hauishii kwa wenye vyeo pekee, bali kila mtumishi ana nafasi ya kuonesha uongozi kupitia uwajibikaji, maamuzi sahihi na namna anavyotekeleza majukumu yake

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa watu (Engagement of People) kwa kueleza kuwa matokeo bora ya Mamlaka yanategemea mchango wa kila mtumishi, ushirikiano baina ya watumishi na utayari wa kubadilishana maarifa na uzoefu katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu.

Katika uboreshaji endelevu (Improvement), amewataka watumishi kutoridhika na namna ambayo kazi zimekuwa zikifanyika kwa mazoea, bali kuendelea kutafuta mbinu bora zaidi za kurahisisha huduma, kuongeza ufanisi na kuimarisha uzoefu wa wananchi wanaohudumiwa na Mamlaka.

Pia amesisitiza umuhimu wa maamuzi yanayotegemea ushahidi (Evidence-based Decision Making), akiwataka watumishi kutumia taarifa, takwimu, kumbukumbu na ushahidi katika kufanya maamuzi na kutatua changamoto badala ya kutegemea dhana au hisia.

Kuhusu usimamizi wa mahusiano (Relationship Management), CPA Dkt. Suluo amesema LATRA inatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, hivyo watumishi wanapaswa kujenga na kudumisha mahusiano mazuri na wananchi, watoa huduma, taasisi za Serikali na wadau wengine wa Sekta ya Usafiri Ardhini.

Aidha, CPA Dkt. Suluo amewataka watumishi kuwa waadilifu wakati wote, hata baada ya muda wa kazi, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, uwajibikaji na weledi. Ameeleza kuwa mwenendo wa mtumishi, akiwa kazini au nje ya mazingira ya kazi, unaweza kuchangia kujenga au kuathiri taswira ya LATRA mbele ya wananchi na wadau.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi walioshiriki kikao hicho, Felichism Tarimo, Afisa Mfawidhi wa Ofisi ya LATRA Karatu, ameishukuru Menejimenti ya LATRA kwa kuendelea kuandaa vikao kazi vya aina hiyo, akisema vina nafasi muhimu katika kuongeza uelewa na ufanisi wa watumishi.

Amesema vikao hivyo vinawakumbusha watumishi misingi muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao, vinawapa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa wenzao, pamoja na kujadili mabadiliko na masuala mapya yanayohusu kazi zao.

Kikao hicho cha siku mbili kimewakutanisha watumishi wa Idara ya Barabara kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu, utoaji wa huduma bora, uadilifu, uwajibikaji na uendelevu katika utoaji wa huduma za udhibiti wa usafiri ardhini.

Ujumbe mkuu wa kikao hicho ni kwamba ubora si jukumu la mtu mmoja wala kitengo kimoja. Kila mtumishi wa LATRA ni sehemu ya QMS, na ubora wa Mamlaka huonekana kupitia huduma anayopokea mwananchi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor