Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAJENGA UWEZO WA WATUMISHI KUSIMAMIA MAZINGIRA, JAMII NA UTAWALA BORA
Imewekwa: 01 Apr, 2026
LATRA YAJENGA UWEZO WA WATUMISHI KUSIMAMIA MAZINGIRA, JAMII NA UTAWALA BORA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inaendesha mafunzo kwa wawakilishi wa watumishi kutoka Idara na Vitengo vya Mamlaka hiyo ili kuwajengea uelewa na uwezo wa kuzingatia Viwango vya Kimataifa wanapotekeleza majukumu yao ili kulinda mazingira na maslahi ya jamii ikiwa ni utekelezaji wa masuala ya Uendelevu wa Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG).

Mafunzo hayo yanafanyika kuanzia Machi 30 hadi Aprili 3, 2026, Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam na yanahusisha watumishi 11 ambao ni machampioni wa utekelezaji wa masuala ya ESG katika Mamlaka hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bw. Athumani Kwikima, Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka LATRA amesema kuwa, mafunzo hayo yataboresha mtazamo wa LATRA katika uhifadhi wa mazingira na amewasihi watumishi waliopatiwa mafunzo kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko ndani ya Mamlaka katika maeneo ya Mazingira, Jamii na Utawala.

“Naamini mafunzo haya yanakwenda kuboresha kabisa mtazamo wetu wa namna tunavyotunza mazingira yetu, ni imani yangu kuwa baada ya mafunzo haya sisi tuliopo hapa tunakwenda kuwa vinara ili kuhakikisha tunalinda mazingira yetu kwa faida ya vizazi vijavyo,” amesema Bw. Kwikima.

Kwa upande wake CPA Njama Moyo, Mratibu wa masuala ya ESG LATRA ameeleza kuwa mafunzo hayo yataiwezesha Mamlaka kutekeleza masuala hayo kwa viwango vya Kimataifa  kupitia maarifa na mbinu bora walizojifunza

“Mamlaka imechukua hatua za haraka kutupatia mafunzo haya ili tuendane na mizani ya Kimataifa, nitoe wito kwa watumishi wenzangu kuwa tuyapokee haya tuliyojifunza kwani sio mapya kutoka kwenye shughuli zetu za kila siku bali ni kuyaweka katika mfumo rasmi ambao tunaweza kujipima, naamini haya mafunzo yanakwenda kuboresha utendaji kazi wetu,” amesema CPA Njama Moyo.

Naye Bi. Rukia Kibwana, Afisa Mfawidhi LATRA, Kituo cha Mabasi Magufuli amesema Mamlaka imekuwa ikitekeleza masuala ya ESG kwa namna mbalimbali ikiwemo kupitia Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo imesaidia kulinda mazingira.

“Zamani tulikuwa tuna tiketi za makaratasi ambayo kwa kweli hazikuwa Rafiki kwa mazingira lakini kwa sasa tuna Mfumo wa Safari Tiketi ambapo mdau anayetaka kusafiri wakati wowote na mahali popote alipo anaingia kwenye Mfumo tiketi.latra.go.tz/ na kukata tiketi yake kielektroni,” amesema Bi. Rukia.

Kwa upande wake, FCPA Dkt. Neema Kiure, mwezeshaji wa masuala ya Maendeleo Endelevu, ameipongeza LATRA kwa kuandaa mafunzo ya hayo akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya Mamlaka katika kuimarisha utekelezaji wa masuala ya maendeleo endelevu na kuendana na viwango vya kimataifa katika sekta ya usafiri ardhini nchini.

“Kufuatia mafunzo haya, ninaiona LATRA ikiwa taasisi ya kuigwa na inayoweza kutajwa Kimataifa kama miongoni mwa taasisi zilizofanikiwa kusimamia usafiri endelevu ardhini kwa ufanisi na kuzingatia misingi ya ESG,” amesema FCPA Dkt. Kiure”

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuleta chachu ya mabadiliko chanya ndani ya LATRA na sekta ya usafiri kwa jumla, ambapo kuanza kufanyiwa kazi kwa dhana hii kutasaidia kuendana na sera za kimataifa, kuboresha mipango na utoaji wa huduma, na hii itasaidia uwepo wa usafiri bora, endelevu na salama nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo