Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa semina ya kuwajengea uwezo Wafanyakazi muhimu wa usalama katika undeshaji wa reli (Safety Critical Workers) ikiwemo madereva na waongoza treni wa Treni ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kuwaongezea ujuzi wa kutimiza majukumu yao kwa uweledi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi utakaosaidia kupunguza ajali zitokanazo na makosa ya kibinadamu.
Hayo yamesemwa na Mha. Moses Nyoni, Afisa Mkaguzi wa Reli Mwandamizi LATRA aliyemuwakilisha Mha. Hanya Mbawala, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Reli LATRA katika semina iliyofanyika Februari 16, 2026 Stesheni ya John Magufuli, Dar es Salaam.
“Semina hii imelenga kuwakumbusha wataalamu wetu majukumu yao pamoja na namna bora ya kuenenda wawapo kazini, hii itasaidia kupunguza makosa ya kibinadamu yanayoweza kusababisha ajali, hivyo madereva na waongoza treni wakiwa kama watu wa mbele katika mfumo wa treni kufanya kazi, tunao wajibu wa kuwaelimisha na kuwakumbusha masuala ya usalama,” amesema Mha. Nyoni.
Vilevile amesema, “Mafunzo haya yatasaidia sana katika kuondoa makosa ya kibinadamu miongoni mwenu kwani makosa hayo husababisha hasara nyingi na kubwa kwa taifa ikiwemo ajali za treni ambazo huharibu miundombinu ya reli na treni yenyewe lakini pia kuepuka kupata harasa za mali na hata kupoteza maisha kwa abiria wanaotumia vyombo hivyo,”
Akizunguza baada ya mafunzo haya Mha. John Ngaraguza, Mkufunzi wa Masuala ya Reli amesema kuwa, semina hiyo imejikita katika kuamsha morali ya kazi, na kupunguza viashiria vinavyoweza kuchochea makosa ya kibinadamu kama vile msongo wa mawazo, uchovu na ufanyaji kazi kimazoea.
“Semina hii imewalenga Madereva wa Treni, waongoza Treni (Train controllers) wanaohusika na Treni ya Kisasa (SGR) ambapo pamoja na yote wamejengewa uwezo wa kuutumia kiufasaha mfumo wa uongozaji treni uliopo kwa sasa,” amesema Ngaraguza.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru LATRA kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani yamewapatia mwanga na kuwafanya wawe tayari zaidi kuitumikia sekta ya reli na taifa kwa jumla ili kuleta maendeleo ya pamoja katika sekta ya usafiri wa reli nchini.

