Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewapa watoa huduma wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani siku 14 kuanzia tarehe 30 Januari, 2026 kuhamia kwenye mifumo ya tiketi mtandao iliyoidhinishwa rasmi na Mamlaka. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha utekelezaji kamili wa Kanuni za Tiketi Mtandao za mwaka 2024 na kuboresha udhibiti wa huduma za usafiri wa abiria nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari Januari 30, 2026, Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, Bw, Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA amesema. mabasi yote yatakayokuwa bado yanatumia mifumo ya tiketi mtandao isiyoidhinishwa hayataruhusiwa kutoa huduma. Aidha, utoaji na uhuishaji wa leseni za usafirishaji wa abiria utazingatia matumizi ya mifumo ya tiketi mtandao iliyoidhinishwa pekee.
“Hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2026 jumla ya mifumo 10 ya tiketi mtandao imekidhi vigezo vya kisheria na kuidhinishwa kuendelea kutoa huduma, huku mifumo mingine ikizuiliwa kutokana na kushindwa kutimiza matakwa ya kisheria licha ya kupewa muda wa kutosha. Tunawasihi watoa huduma ambao bado hawajakamilisha taratibu za uidhinishaji kufanya hivyo ili waruhusiwe kutoa huduma kwa mujibu wa Sheria”, ameeleza Bw. Pazzy.
Bw. Pazzy ameitaja mifumo iliyokidhi vigezo na kuidhinishwa kuwa ni AB Connect, Busbora, MySafari tiketi, Iyishe Company Limited, Msafiri, Baspoa, Otapp, Afritech, Voltic Tanzania Limited na Web e-ticketing.
Ameongeza kuwa, ili mfumo upate kibali unapaswa uwe unamilikiwa na taasisi ya Serikali, chama cha ushirika au kampuni iliyosajiliwa Tanzania, uwe umeunganishwa na mfumo wa usimamizi wa malipo ya mapato wa kielektroni, uwe una uwezo wa kuunganishwa na mifumo ya Mamlaka, Mfumo Mkuu wa Tiketi Mtandao, na mfumo wowote kama inavyohitajika, uwe umeidhinishwa na mamlaka zinazohusika, uwe wa kitanzania, uwe na mmiliki mwenye wafanyakazi wenye taaluma husika na uwe na ulinzi dhidi ya vamizi za kimtandao.
Kwa upande mwingine, LATRA imewakumbusha wasafirishaji kuhakikisha wanatumia wahudumu wa mabasi waliosajiliwa na Mamlaka hiyo na kuhakikisha kila abiria anasafiri akiwa na tiketi mtandao, abiria nao wametakiwa kununua tiketi kupitia mifumo iliyoidhinishwa na kutumia programu ya LATRA App kuhakiki tiketi na nauli halali, huku wakihimizwa kuwasilisha malalamiko yao kwa watoa huduma na kama hawajaridhika na suluhisho la msafirishaji wawasilishe LATRA kwa kupiga bure bila malipo kwa namba 0800110019 au 0800110020 au kupitia mfumo wa e-Mrejesho.
Hatua ya kuimarisha matumizi ya mifumo ya tiketi mtandao inalenga kuwawezesha wasafirishaji kupata mapato kwa ufanisi bila kupitia watu wa kati, kuwasaidia abiria kununua tiketi kwa uwazi na urahisi, pamoja na kuzuia vitendo vya ulanguzi wa tiketi. Pia,matumizi ya mifumo hiyo yataisaidia Serikali kusimamia sekta ya usafiri kwa ufanisi zaidi na kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

