Mamlaka ya Udhibiti usafiri Ardhini (LATRA) imewataka watoa huduma za usafiri wa mabasi ya mijini (Daladala) zinazotoa huduma barabara ya Kilwa ifikapo Julai Mosi, 2026 kusitisha zoezi la kupakia na kushusha abiria katika maeneo yanayohudumiwa na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Pili kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika njia hiyo kupitia huduma za usafiri wa BRT.
Agizo hilo limetolewa na CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, alipofanya ziara katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Kwanza na ya Pili njia ya Kimara kwenda katikati ya mji na Mbagala kwenda katikati ya mji Juni 15, 2026 ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza rasmi kwa huduma za kibiashara za BRT Awamu ya Pili zinazotarajiwa kuanza Julai 1, 2026, baada ya kipindi cha majaribio.
CPA, Dkt. Suluo amesema kuwa kuendelea kwa daladala kupakia na kushusha abiria katika maeneo ya miundombinu ya BRT kunasababisha mwingiliano wa huduma na kuathiri ufanisi wa huduma hizo ambazo Serikali imewekeza kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa umma kwa wananchi.
“Abiria wanaotoka Mkuranga, Tuangoma na maeneo mengine ya pembezoni watashuka katika Kituo cha Mbagala Rangi Tatu na kuunganisha safari zao kwa kutumia mabasi ya mwendokasi kuelekea Kariakoo, Kivukoni na maeneo mengine ya katikati ya jiji. Vivyo hivyo, daladala zinazofanya safari kati ya Mbagala, Kariakoo na Kivukoni zinapaswa kuzingatia vituo vya mwisho vilivyopangwa bila kusimama njiani kupakia au kushusha abiria ndani ya njia ya mwendokasi,” amesema CPA, Dkt. Suluo.
Pia amesema Mamlaka tayari imefanya maboresho ya ada za leseni yatakayoanza kutumika Julai 2026, ambapo baadhi ya malipo yatawezesha watoa huduma kutumia miundombinu ya vituo bila kulazimika kulipa gharama za ziada kila wanapoingia katika vituo hivyo.
Amebainisha kuwa, kwa sasa huduma za BRT Awamu ya Pili zinazotolewa na Kampuni ya MOFAT Limited zinatumia mabasi 50 pekee kati ya mabasi 200 yaliyowekezwa na kampuni hiyo. Hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa huduma zinazofanana katika njia hiyo, jambo linalopunguza ufanisi wa uwekezaji uliofanyika.
Kwa upande wake Bw. Said Tunda, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wadau wote wa sekta ya usafiri kunufaika na mfumo wa BRT bila kuathiri ajira zao.
Ameongeza kuwa, juhudi zinaendelea kufanyika kuondoa mwingiliano usio wa lazima katika utoaji wa huduma za usafiri, huku ukarabati wa baadhi ya vituo vya mwendokasi vilivyoharibika ukiendelea na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai 2026 ili kuboresha zaidi huduma za usafiri kupitia BRT Awamu ya Pili.
“Tunachofanya sasa ni kuandaa sekta hii ili wale wote waliokuwa wakifanya biashara hiyo hapo awali waweze kuhamia katika mfumo wa kisasa bila kupoteza ajira zao. Badala yake, mfumo huu utasaidia kuongeza ajira rasmi na kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema Tunda.
Naye Bw. Mohamed Kassim, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MOFAT Limited, amesema changamoto zinazoikabili kampuni hiyo zimechangia kushindwa kufikia kiwango cha huduma kilichokusudiwa, jambo ambalo pia limeathiri fursa za ajira.
Amefafanua kuwa iwapo mabasi yote 200 yangeanza kutoa huduma kwa wakati mmoja, kampuni ingeweza kuajiri wafanyakazi kati ya 1,200 na 1,300, tofauti na hali ya sasa ambapo mabasi 50 pekee ndiyo yanayotoa huduma na kutoa ajira kwa wafanyakazi 423.
LATRA, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na DART, inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha mfumo wa usafiri wa umma unaimarika, unaendeshwa kwa ufanisi na kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

