Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA KUONGEZA USHIRIKIANO KIUDHIBITI KATI YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI
Imewekwa: 24 Aug, 2022
LATRA KUONGEZA USHIRIKIANO KIUDHIBITI KATI YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI

Na. Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendesha kikao kazi na Wataalamu kutoka Taasisi ya Serikali ya Afrika Kusini inayosimamia masuala ya Usafirishaji Nje ya Mipaka (Cross Border Road Transport Agency (C-BRTA) - South Africa) katika makao makuu ya LATRA Dar es Salaam kwa lengo la kujadili na kujifunza namna shughuli za Udhibiti Usafiri Ardhini zinavyotekelezwa nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amesema Kikao hicho kitaongeza ushirikiano uliokuwepo baina ya nchi hizo mbili.

“Ushirikiano kati ya nchi hizi mbili umekuwapo kwa muda mrefu, nadhani mnapajua Morogoro ambapo ndipo Mashujaa wa Afrika ya Kusini waliweka kambi. Hivyo kikao kazi hiki kitaongeza na kudumisha ushirikiano uliokuwapo kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata kiutamaduni,” amesema CPA Suluo.

Naye Meneja Mipango na Udhibiti kutoka C-BRTA Afrika ya Kusini Wakili Khatu Mafuraha ambaye pia ni Mkuu wa Msafara huo, ameishukuru LATRA kwa mapokezi na kuridhia kikao kazi hiko ambapo amesema kitaongeza Ufanisi katika taasisi yao pindi watakaporudi.

“Nawashukuru kwa kukubali kukaa nasi na kushiriki katika kikao kazi hiki ambapo mbali na kuwa ni moja ya ishara ya ushirikiano baina ya nchi zetu (Tanzania na Afrika Kusini), pia kitatusaidia kujua mbinu na mikakati itakayowezesha kuongeza ufanisi katika shughuli za udhibiti nchini kwetu, hivyo tunategemea kujifunza mengi kutoka kwenu,” amesema Mafuraha.

Katika kikao kazi hicho, wajumbe hao wameelezwa shughuli za Mamlaka pamoja na namna LATRA inavyotekeleza Sheria na Kanuni za Udhibiti Usafiri Ardhini hapa nchini na kimehudhuriwa na wajumbe kutoka C-BRTA Afrika Kusini pamoja na Menejimenti ya Mamlaka.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo