Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Morogoro imetoa elimu ya rushwa kwa maafisa usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu (Pikipiki na Bajaji) wanaotoa leseni za vyombo vya usafiri wa kukodi kwa niaba ya Mamlaka ikiwa ni sehemu ya jitihada za makusudi za LATRA katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa, pamoja na kuimarisha uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za usafiri ardhini.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Februari 11, 2026 mkoani Morogoro Bw. Andrew Mlacha, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Morogoro, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha huduma za usafiri zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo, huku wananchi wakipata huduma bora bila usumbufu wala mianya ya vitendo visivyo halali.
Aidha, Bw. Mlacha amesisitiza umuhimu wa kutumia mifumo rasmi ya malipo, akieleza kuwa waombaji wa leseni wanapaswa kufanya malipo kupitia namba maalumu ya malipo (Control Number) ili kuepuka malipo ya ziada au yasiyo rasmi yanayokiuka viwango vilivyowekwa na Mamlaka.
“Serikali imeweka mifumo rasmi ya malipo kwa kutumia namba maalumu ya malipo (Control Number), hivyo hakuna wakala anayeruhusiwa kupokea fedha taslimu mkononi kinyume na utaratibu uliowekwa. Endapo atabainika yeyote kukiuka taratibu hizo, hatua kali zitachukuliwa mara moja ikiwemo kufutiwa leseni ya uwakala,” amesema Bw. Mlacha.
Vilevile, mawakala hao wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kuvaa sare maalumu pamoja na vitambulisho vya kazi wanapotekeleza majukumu yao, ili waweze kutambulika kwa urahisi na kuepusha migogoro isiyo ya lazima baina yao na wananchi.
Aidha, wamehimizwa kutumia lugha za staha katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakikumbushwa kuwa kauli njema ni chachu ya kuboresha huduma kwa wananchi, wakati lugha isiyo na staha huathiri utoaji wa huduma na kuchochea migogoro kati ya Mamlaka na watoa huduma.
Kwa upande wao, maafisa usafirishaji walioshiriki mafunzo hayo wameipongeza LATRA pamoja na Serikali kwa kuwawezesha kupata elimu hiyo muhimu, wakieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji kazi wao na kutatua changamoto zilizokuwepo awali katika utoaji wa leseni.
Serikali kwa kushirikiana na LATRA inaonesha dhamira ya dhati ya kuendelea kuimarisha uwajibikaji, nidhamu na ufanisi katika sekta ya usafiri ardhini, hususan huduma za vyombo vya usafiri wa kukodi ambazo zinaendelea kukua kwa kasi mkoani Morogoro na nchini kwa jumla.

