Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA, POLISI KUKOMESHA UKIUKWAJI WA MASHARTI YA LESENI
Imewekwa: 22 Jul, 2022
LATRA, POLISI KUKOMESHA UKIUKWAJI WA MASHARTI YA LESENI

Na. Mambwana Jumbe

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Mhe. Jumanne Sagini (MB) ameelekeza Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kushirikiana kupitia idadi ya magari madogo yaliyopewa leseni za usafirishaji na kutathmini ukiukwaji wa masharti ya leseni nchi nzima na kuwachukulia hatua za kisheria madereva na wamiliki wanaokiuka mashari ya leseni zao.

Mhe. Sagini amesema hayo Julai 22, 2022 kwenye mkutano na waandishi wa habari kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jijini Dar es Salam.

Katika mkutano huo, Mhe Sagini amesema kuwa Serikali inataka kuona vyombo vinavyotembea barabarani vinazingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani, vilevile kuendelea kutoa elimu kwa abiria na kushauri kutumia usafiri wa mabasi au vyombo vingine vya moto vilivyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria, “kwenye hili nawaomba abiria ambao ni wananchi wenzetu wasiwe sehemu ya kukiuka sheria”.

Aidha, Mhe. Sagini amewasihi wasafirishaji wenye magari yanayokidhi vigezo vya kusafirisha abiria kuomba leseni kwenye maeneo yenye uhitaji kama vile mikoa ya Simiyu, Kagera, Kigoma, na kadhalika ili kupunguza adha ya usafiri katika maeneo hayo.

Vilevile amesisitiza kuwa LATRA na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala muhimu ya usalama kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Pia Mhe. Sagini ameipongeza kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Simiyu ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. David Kafulila kwa kuchukua hatua za kudhibiti matumizi ya magari yaliyosajiliwa kama teksi yanayokiuka sheria na kubeba abiria wa masafa marefu. Uamuzi huo ni baada ya kamati kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa magari hayo yalikuwa yakikiuka sheria za usalama barabarani na masharti ya leseni kwa kiasi kikubwa ikiwemo kubeba abiria wengi kuliko uwezo wa gari, kuendesha kwa mwendokasi pamoja na ubovu wa magari.

Naye Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amemshukuru Mhe. Sagini na amesema kuwa itashirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau wengine kutoa elimu kwa watoa huduma za usafirishaji na wananchi, kufanya tathmini na kuchukua hatua kwa wanaokiuka sheria.

“LATRA inafanya kaguzi mbalimbali ikiwemo kukagua viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa na masharti ya leseni. Kwa upande wa mabasi yanayoenda mikoani tumeshachukua hatua na kwa sasa hivi hatutoi leseni bila basi kuwa limeunganishwa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari –VTS. Kanuni za Leseni za usafirishaji kwa magari ya abiria za mwaka 2020 zinataka abiria kupatiwa tiketi ya kielektroni, ambapo kwa sasa tunaendelea na kampeni kuhakikisha kuwa mabasi yanatoa tiketi hizo.”

Aidha ameeleza kuwa, suala la ajali ni mtambuka hivyo Mamlaka itashirikiana na viongozi wa mikoa mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la ajali.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania Wilbroad Mutafungwa, Maofisa wa jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barababani, Wakuu wa usalama barabarani kutoka Kinondoni, Ilala na Temeke pamoja na maofisa wa LATRA.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo