Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA, POLISI KUONGEZA UDHIBITI WA AJALI NCHINI
Imewekwa: 18 Jul, 2023
LATRA, POLISI KUONGEZA UDHIBITI WA AJALI NCHINI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inategemea kuongeza na kudumisha ushirikiano uliopo kati yake na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ili kuhakikisha udhibiti wa usalama barabarani unakuwa thabiti na wenye tija kwa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini.

Hayo yamesemwa na Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA katika semina ya mafunzo kwa Wakuu wa Usalama Barabarani Mkoa (RTOs) na Wakaguzi wa magari nchini, semina hiyo ya siku tatu imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa kampuni ya Superdoll Julai 17, 2023 na kufunguliwa na CP Awadhi H. Awadhi, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Tanzania.

Akizungumza baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo, Bw. Kahatano amesema, “Kwakuwa elimu inayotolewa hapa inawafikia moja kwa moja Wakuu wa Usalama Barabarani Mkoa ambao ndio wasimamizi wakuu katika Mikoa yote Tanzania, pia wapo wakaguzi ambao ni watendaji, hii itasaidia kuongeza udhibiti wa usalama barabarani kwa kiasi kikubwa,” amesema Bw. Kahatano.

Aidha, Bw. Kahatano ameeleza kuwa ushiriki wa LATRA katika semina hiyo itaongeza ushirikiano ambao umekuwepo kwa muda mrefu kati ya LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na hivyo kuleta tija katika utendaji.

“Ni mategemeo yangu kuwa ushirikiano uliopo baina yetu na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani utaongezeka zaidi baada ya semina hii, kwani tumepata fursa nzuri ya kuwezesha mafunzo haya na pia tunapata nafasi ya kueleza majukumu yetu kama LATRA na maeneo ambayo tunahusiana moja kwa moja na Jeshi la polisi,” ameeleza Bw. Kahatano.

Kwa upande wake CP Awadhi H. Awadhi ameishukuru LATRA pamoja na wadau wengine ambao wameshiriki kuwezesha semina hii ya mafunzo kwa Wakuu wa Usalama Barabarani Mkoa (RTOs) na wakaguzi wa Magari nchini.

“Nipende kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza LATRA pamoja na wadau wengine kama TIRA na TRA  ambao muda wote wamekuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ili kuhakikisha kwa pamoja tunadhibiti usalama barabarani, pia kwa kutuwezesha ili kufanikisha utoaji wa mafunzo haya kwa Wakuu wa Usalama Barabarani Mkoa (RTOs) na wakaguzi wa Magari nchini,” amesema CP Awadhi.

Lengo la semina hiyo ni kuwaongezea ujuzi wa ukaguzi wa vyombo vya moto na ufuatiliaji wa hali ya usalama kwa Wakuu wa Usalama Barabarani Mkoa (RTOs) na wakaguzi wa Magari nchini ili kuhakikisha uwezekano wa kupata ajali unapunguzwa kwa kiasi kikubwa.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo